Askofu Mkuu wa Canterbury awasili Cameroon kwa ziara ya kichungaji
Askofu Mkuu wa Canterbury, Dame Sarah Mullally, amewasili nchini Cameroon kwa hatua ya pili ya ziara yake ya mataifa mawili barani Afrika.
Hapo jana alipokelewa na viongozi wa serikali ya Cameroon, maafisa wa Kanisa la Anglikana pamoja na Kamishna Mkuu wa Uingereza nchini humo.
Akiwasili katika uwanja wa ndege wa Yaoundé, alisema anafurahia kutembelea taifa hilo la Afrika ya Kati katika ziara yake ya siku kumi barani humo.
"Ni heshima kubwa kwangu kuwa hapa Cameroon. Hii ni mara yangu ya kwanza kutembelea Afrika kama Askofu Mkuu wa Canterbury," aliwaambia waandishi wa habari.
Aliongeza kuwa yuko nchini humo kwa ziara ya kichungaji ya kuomba, kuabudu pamoja na Kanisa la Anglikana, kutembea bega kwa bega na waumini wake, na kuwatia moyo katika huduma yao.
Kabla ya kuwasili nchini humo, Dame Sarah alikuwa Ghana kwa siku tano ambapo alikutana na waumini wa Kanisa la Anglikana na kuimarisha uhusiano wao na Kanisa la England.
Akiwa huko pia alithibitisha tena dhamira ya kanisa hilo ya kutenga pauni milioni 100 katika mfuko wa kushughulikia athari za kihistoria za ushiriki wa Kanisa la England katika biashara ya utumwa kupitia Bahari ya Atlantiki.
Katika ziara yake ya siku tano nchini Cameroon, atatembelea miji minne, ikiwemo Buea na Limbe katika eneo la Kusini Magharibi linalozungumza Kiingereza, ambako mgogoro wa mapigano umeendelea kwa karibu muongo mmoja.
"Katika kipindi hiki cha migogoro mikubwa duniani na mateso yanayoendelea hapa Cameroon, nimekuja nikiwa na ujumbe wa Injili," alisema, akieleza kuwa ujumbe huo ni wa amani.
Akiwa Buea, atatembelea taasisi inayotoa mafunzo kwa wauguzi na wakunga. Uhusiano wake na taaluma ya uuguzi unatokana na kazi yake ya awali kama muuguzi katika Huduma ya Afya ya Taifa ya Uingereza (NHS), ambako alipandishwa vyeo hadi kushika nafasi za juu.Siku ya Jumapili, Askofu Mkuu huyo mwenye umri wa miaka 64 atahubiri katika Bishopscourt jijini Douala, makao makuu ya Dayosisi ya Cameroon. Pia atatembelea makanisa mbalimbali na kukutana na viongozi wa dini katika jiji hilo.
Atakaporejea Yaoundé siku ya Jumatatu, atatembelea taasisi nyingine za kidini na kufanya mazungumzo na viongozi wa serikali kabla ya kuondoka nchini Cameroon siku ya Jumanne.