Rais wa Nigeria aagiza nyongeza ya mishahara ya asilimia 80 kwa askari wa vyeo vya chini

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanajeshi wa Nigeria wanatarajiwa kupata nyongeza ya mishahara ya hadi asilimia 80 – ikiwa ni mara ya pili kwa mishahara yao kuongezwa ndani ya mwezi mmoja – kutokana na kile ambacho Rais Bola Tinubu anakitaja kuwa ni "shukrani kubwa" ya serikali kwa wale wanaopambana na vitisho vikubwa vya usalama vinavyolikabili taifa.
Mwezi Julai, Waziri wa Ulinzi aliongeza mishahara ya kila mwezi ya askari wa ngazi ya chini kabisa kutoka dola 36 (pauni 27) hadi dola 73.
Kufuatia uamuzi wa Rais, sasa watapokea dola 132 kuanzia mwezi Septemba.
Hatua hii ni sehemu ya juhudi za Tinubu za kudhibiti vurugu zinazosababishwa na makundi mbalimbali yenye silaha, yakiwemo makundi ya wapiganaji wa Kiislamu na magenge ya uhalifu yanayojihusisha na utekaji nyara, ambayo kwa ndani yanajulikana kama "majambazi".
Mwezi uliopita, aliamuru kuajiriwa kwa wanajeshi wa ziada 28,000 na kuanzishwa kwa vikosi vipya vinne vya jeshi.
Hali ya ukosefu wa usalama inayoendelea nchi nzima imekuwa suala kuu la kisiasa kuelekea uchaguzi wa mwaka 2027.


