Comey ashtakiwa kwa kumtishia maisha Trump mtandaoni
Aliyekuwa mkurugenzi wa shirika la kijasusi la Marekani, James Comey, ameshtakiwa kwa kumtishia maisha Rais wa Marekani Donald Trump, shitaka rasmi linalotokana na picha aliyowahi kushiriki kwa muda mfupi kwenye mitandao ya kijamii
Picha hiyo iliyochapishwa kwenye mtandao wa Instagram mwaka jana ilionyesha magamba ya baharini yaliyopangwa kuunda namba “86 47”. ni istilahi ya mtaani inayomaanisha “kuondoa” au “kuondoa kabisa”.
Comey amesisitiza kuwa hakujua maana ya namba hizo kwenye picha, lakini Trump na maafisa wengine wa utawala wamesema chapisho hilo lilikuwa tishio dhidi ya rais wa 47.
Akijibu mashtaka hayo Jumanne, Comey alisema: “Bado sina hatia, bado siogopi, na bado nina imani na mahakama huru ya shirikisho.”
Katika mkutano na waandishi wa habari kutangaza shitaka hilo, Mkurugenzi wa FBI Kash Patel alisema kuwa kama aliyekuwa mkuu wa taasisi hiyo, Comey “alijua vizuri athari na matokeo ya kufanya chapisho kama hilo.”
Comey alifutwa kazi na Trump katika muhula wake wa kwanza baada ya kuanzisha uchunguzi kuhusu uingiliaji wa Urusi katika uchaguzi wa urais wa Marekani wa 2016.
Tangu wakati huo, Trump amekuwa akitaka mara kwa mara mashtaka kufunguliwa dhidi yake — na mashtaka ya Jumanne ni jaribio la pili la utawala wake kufanya hivyo.
Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, Comey anakabiliwa na mashtaka ya kutoa vitishio dhidi ya rais na kusambaza tishio katika biashara ya kati ya majimbo. Kila shitaka lina adhabu ya hadi miaka 10 jela.
Maafisa wa kijasusi wa Secret Service walimhoji Comey mwezi Mei mwaka jana kuhusu picha hiyo ya magamba ya baharini.
Comey alifuta chapisho hilo la Instagram, akisema katika maelezo yaliyofuata kuwa “alidhani [magamba ya baharini] yalikuwa ujumbe wa kisiasa.”
Trump, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akimkosoa Comey, alisema kuhusu chapisho hilo kwamba “hata mtoto anajua lilimaanisha nini.”
Baadhi ya wataalamu wa sheria wamesema shitaka hilo linaonekana dhaifu na limeibua maswali mapya kuhusu juhudi za Wizara ya Sheria kuwalenga wale wanaochukuliwa kuwa wapinzani wa kisiasa wa Trump.
Chapisho la Comey kwenye mitandao ya kijamii linaweza kutazamwa na mahakama kama uhuru wa kujieleza unaolindwa na Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Marekani, wataalamu walisema.
Hii ni mara ya pili kwa wizara ya sheria kumfungulia Comey mashtaka.
Comey alishtakiwa na baraza la majaji wakuu wa shirikisho mwishoni mwa Septemba kwa madai kwamba alidanganya bungee la Congress wakati akitoa ushahidi wake Septemba 2020 na kuzuia mchakato wa bunge.
Mashtaka hayo yalikuja siku chache baada ya Trump kumtaka mkuu wa vyombo vya sheria nchini kuchunguza kwa nguvu zaidi wapinzani wake wa kisiasa, akiwemo Comey.
Comey alikana mashtaka hayo wakati wa kufikishwa kwake mahakamani kwa muda mfupi Oktoba kabla ya kesi hiyo kufutwa mwezi Novemba.
Jaji Cameron Currie alitupilia mbali shtaka dhidi ya Comey kutokana na uteuzi “usio halali” wa mwendesha mashtaka Lindsey Halligan.
Hata hivyo, jaji huyo aliacha wazi uwezekano kwa serikali kujaribu tena.
Mapema Jumanne, jaji mwingine aliamua kwamba aliyekuwa mwendesha mashtaka wa shirikisho Maurene Comey — ambaye ni binti wa James Comey — anaweza kuendelea na kesi yake ya kupinga kufutwa kazi kwake na utawala wa Trump.