Mamlaka zichunguze ukatili wa polisi dhidi ya waandamanaji Tanzania - Amnesty International

Shirika la Amnesty International limezitaka mamlaka za Tanzania kufanya uchunguzi wa haraka, huru na wa kina kuhusu matumizi ya nguvu kupita kiasi na zisizo za lazima yaliyofanywa na polisi dhidi ya waandamanaji siku ya uchaguzi mkuu nchini humo.
Haya yanajiri baada ya ripoti kuwa watu wawili wameuawa na kadhaa kujeruhiwa.
Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa Kanda wa Amnesty International kwa Afrika Mashariki na Kusini, Tigere Chagutah, alisema:
“Taarifa za raia mmoja na askari polisi mmoja wameuawa katika maandamano ya siku ya uchaguzi nchini Tanzania ni za kusikitisha sana. Kuna hatari kubwa ya kuongezeka kwa machafuko tunazihimiza mamlaka za polisi kujizuia na kuepuka kutumia nguvu zisizo za lazima au kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.”
“Mamlaka za Tanzania lazima zifanye uchunguzi wa kina, huru na wa haraka kuhusu matumizi yasiyo halali ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji, na kuhakikisha kwamba wahusika wote wanawajibishwa ipasavyo.”
Chagutah pia alionya kwamba usumbufu wa huduma za intaneti uliyoripotiwa nchini kote unaweza kuongeza zaidi hali ya taharuki.
“Mamlaka zinapaswa kuhakikisha upatikanaji wa taarifa bila vizuizi, mtandaoni na nje ya mtandao. Ni muhimu huduma ya intaneti irejeshwe kikamilifu na vyombo vya habari vya ndani na vya kimataifa viruhusiwe kuripoti kwa uhuru kuhusu uchaguzi. Serikali ina wajibu wa kikatiba kulinda na kuheshimu haki za binadamu za wote kabla, wakati na baada ya uchaguzi,” aliongeza.
Soma pia:







































