Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja , Iran yasema haiwezi kuzuiwa kwa vikwazo vya ardhini huku Marekani ikiongeza vikwazo vya kiuchumi.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araqchi, amesema kuwa, kuizuia Iran kupitia vikwazo vya ardhini ni jambo ambalo haliwezekani kutokana na ukubwa wa nchi hiyo.

Muhtasari

Iran yasema haiwezi kuzuiwa kirahisi kwa vikwazo vya ardhini

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Kiongozi wa upinzani Zambia ashtakiwa rasmi kwa uhaini

    Kiongozi wa upinzani nchini Zambia, Brian Mundubile, pamoja na washirika wake zaidi ya 12, walifikishwa mahakamani hapo jana wakikabiliwa na mashtaka ya kupanga njama za kuipindua serikali, huku mahakama kuu ikitarajiwa kuanza kusikiliza kesi yao ya uhaini.

    Kulingana na hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamanihapo jana, Mundubile na wenzake wanatuhumiwa kupanga njama za kuipindua serikali kati ya mwezi Aprili na Agosti 2026.

    Mundubile na mgombea mwenza wake katika uchaguzi, Makebi Zulu, walikamatwa na kuhojiwa kuhusu tuhuma za uhaini muda mfupi baada ya uchaguzi wa urais kufanyika mwezi wa Agosti. Wawili hao walidai kuwa uchaguzi huo uliibwa.

    Rais Hakainde Hichilema alishinda uchaguzi huo na amekanusha madai ya kuwepo kwa udanganyifu wowote.

    Kulingana na hati ya mashataka, Mundubile na mfanyabiashara mmoja walitoa fedha kwa ajili ya kuwapeleka watu watano nchini Urusi kupata mafunzo ya kijeshi, kwa lengo la kutekeleza mpango wa kuipindua serikali.

    Wakili wa upande wa utetezi, Sakwiba Sikota, amesema mashtaka hayo hayana msingi na kwamba upande wa mashtaka unafanya uchunguzi wa kubahatisha ili kutafuta ushahidi wa kuwashtaki.

    Sikota amesema kesi hiyo inatarajiwa kuanza kusikilizwa mapema mwakani.

    Awali, Mundubile alikanusha mashtaka hayo ya uhaini na kusema kuwa yanasukumwa na sababu za kisiasa.

    Soma pia:

  2. Marekani yaongeza vikwazo dhidi ya mtandao wa kifedha wa Iran

    Utawala wa Rais Donald Trump umeiwekea Iran vikwazo vipya, ikilenga watu na taasisi kadhaa ambazo Marekani inazituhumu kuhusishwa na mfumo wa kifedha wa siri wa Iran, unaojulikana kama “Shadow Banking System”, kulingana na taarifa iliyochapishwa hapo jana kwenye tovuti ya Wizara ya Fedha ya Marekani.

    Wizara ya Fedha ya Marekani imewaongeza watu wanane wenye uhusiano na Iran pamoja na taasisi 22 zilizoko Iran, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Uturuki na Hong Kong kwenye orodha ya waliowekewa vikwazo.

    Wizara hiyo imesema kuwa Mtandao wa Utekelezaji wa Uhalifu wa Kifedha (FinCEN) umebaini shughuli za kifedha zenye thamani ya takribani dola bilioni 14.7 kati ya Januari 2025 na Agosti 2026, ambazo zinaaminika kuhusishwa na mfumo huo wa kifedha wa siri wa Iran.

    Taarifa hiyo pia imesema kuwa Kituo cha Ubadilishanaji wa Fedha na Dhahabu cha Iran, kilichoanzishwa takribani miaka mitatu iliyopita kwa idhini ya Benki Kuu ya nchi hiyo, kimeongezwa kwenye orodha ya waliowekewa vikwazo.

    Kulingana na Wizara ya Fedha ya Marekani, mfumo wa kifedha wa siri wa Iran hutumika kuhamisha fedha zinazotokana na biashara ya kimataifa ya nchi hiyo, huku Kituo cha Ubadilishanaji wa Fedha cha Iran kikifanya kazi kama mpatanishi na kuwezesha rasilimali hizo za kifedha kufika kwenye maeneo yanayokusudiwa ndani ya Iran.

    Vikwazo hivyo vya kiuchumi vya Marekani, ambavyo vimekuwa vikiongezwa katika miezi ya hivi karibuni, ni sehemu ya kampeni inayoendelea ya kuitenga Iran kiuchumi, ili kudhibiti maslahi yake ya kifedha pamoja na mitandao yake ya kifedha katika mataifa mbalimbali duniani.

    Soma pia:

  3. Iran yasema haiwezi kuzuiwa kwa vikwazo vya ardhini

    Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araqchi, amesema kuwa, kuizuia Iran kupitia vikwazo vya ardhini ni jambo ambalo haliwezekani kutokana na ukubwa wa nchi hiyo, pamoja na uhusiano na miingiliano iliyopo kati ya majimbo yake, miji na jamii zinazoishi katika maeneo ya mpakani.

    “Kuizuia Iran kupitia vikwazo vya ardhini ni jambo ambalo karibu haliwezekani, kutokana na ukubwa wa nchi yetu na idadi kubwa ya majimbo, ambayo kila moja lina uwezo na rasilimali tofauti. Majimbo hayo yana uhusiano mpana na majimbo jirani katika nchi zinazopakana na Iran, ikiwemo shughuli nyingi za usafiri, uhusiano wa kijamii kati ya wananchi pamoja na mizizi ya kihistoria na kitamaduni inayowaunganisha watu wa pande zote za mipaka,” alisema Araqchi.

    Aidha, Waziri huyo wa Mambo ya Kigeni alisema kuwa kwa maoni yake, Tehran inapaswa kuendelea na diplomasia itakayosaidia kupunguza vikwazo vinavyoikabili taifa hilo.

    “Njia bora ya kukabiliana na shinikizo hizi ni kuhakikisha kuwa vikwazo havifikii malengo yake, ili wanaoviweka watambue kuwa njia hiyo haifanyi kazi na haitafanya kazi.”

    Kulingana na kiongozi huyo, wanaitaka Iran iwe na uwezo wa kustahimili vikwazo vyote,ili kuiwekea Iran vikwazo isiwe na maana tena.

    “Hakuna ambaye anafaa kufikiria kuwa anaweza kuilazimisha Iran kujisalimisha kwa kuongeza shinikizo la kiuchumi na vikwazo.”

    Soma pia:

  4. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Jumanne ya leo