Iran yataka kuondolewa kwa vikwazo vya kijeshi dhidi ya Yemen na kuanza kwa mazungumzo
Asubuhi ya Ijumaa, Septemba 10, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilitoa taarifa kuhusu hali ya vita nchini Yemen, ikitaka kukomeshwa kwa vizuizi vya kijeshi dhidi ya nchi hiyo na kuanza kwa mazungumzo.
Taarifa hiyo, iliyochapishwa na shirika la habari la serikali ya Iran, IRNA, ilisema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka maslahi ya ulimwengu wa Kiislamu yazingatiwe, hasa wakati eneo la Asia Magharibi linakabiliwa na kile ilichokiita “uovu, ukatili na upanuzi usio na kifani wa utawala wa Kizayuni kwa ushirikiano na Marekani.”
Iran ilisema kuwa “suluhisho la masuala ya Yemen haliwezi kupatikana kupitia kuendelea kwa vikwazo na mashambulizi ya kijeshi.”
Mwisho wa taarifa hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilisisitiza “haja ya haraka ya kurejesha mazungumzo, kwa kuzingatia ramani ya njia iliyokubaliwa, na kutekeleza masharti yake.” Ilisema Tehran iko “tayari kwa juhudi zozote katika suala hili.”
Taarifa ya Iran ilitolewa saa chache baada ya kuripotiwa kuwa Wahouthi walikuwa wakisonga mbele katika maeneo kadhaa, yakiwemo karibu na bandari ya Mokha nchini Yemen, na kuwasukuma nyuma wanajeshi wa serikali ya Yemen wanaopokea msaada wa kijeshi kutoka Saudi Arabia.
Alhamisi, Septemba 10, pia kuliripotiwa kuwa vikosi vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia na washirika wake vilijiondoa katika bandari nyingine ya pwani katika eneo hilo, Dhubab.
Kutekwa kwa Mokha kunaweza kuimarisha uwezo wa Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran kudhibiti njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta na bidhaa.
Mokha iko karibu na Mlango wa Bab-el-Mandab, unaounganisha Bahari ya Shamu na Bahari ya Hindi.