Baada ya wikendi ya mashambulizi yaliyoratibiwa kote Mali na wapiganaji wanaotaka kujitenga na wanamgambo wa Kiislamu, vikosi vya Urusi vilivyoko
nchini humo vikisaidia kuilinda serikali ya kijeshi vimethibitisha kuwa
vimeondoka katika mji wa kaskazini wa Kidal.
Katika mfululizo wa machapisho kwenye mitandao ya kijamii, Kikosi cha
Afrika cha Urusi kilisema "wameondoka katika eneo hilo" pamoja na
wanajeshi wa Mali.
Kundi la Azawad Liberation Front (FLA) linalotaka kujitenga lilisema
Jumapili kwamba wanajeshi wa Urusi wamekubali kujiondoa, na kudai udhibiti wa
Kidal, wakitangaza "sasa iko huru".
Mali imekabiliwa na uasi kwa miaka mingi kutoka kwa waasi wanaotaka
kujitenga kaskazini, na makundi yenye uhusiano na al-Qaeda na kundi la Islamic
State.
Siku ya Jumamosi, milipuko na milio ya risasi iliripotiwa katika
sehemu nyingi za Mali, ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Bamako.
Mashambulizi pia yaliripotiwa katika miji ya kati ya Sevare na Mopti,
pamoja na Gao na Kidal kaskazini, kwenye ukingo wa kusini wa jangwa la Sahara.
Huko Kati - mji ulio karibu na mji mkuu na makao makuu ya kambi kubwa ya
kijeshi - Waziri wa Ulinzi wa Mali Sadio Camara aliuawa katika
shambulio la bomu la gari la kujitoa mhanga nyumbani kwake.
Ripoti zinaonyesha kuwa mashambulio ya FLA yalifanyika katika maeneo ya
kaskazini yanayotawaliwa na Watuareg, huku kundi la jihadist Jama'at Nusrat
al-Islam wal-Muslimin (JNIM) likifanya mashambulizi katika maeneo mengi.
Mapigano yalianza tena huko Kidal siku ya Jumapili, lakini muda mfupi
baadaye, msemaji wa FLA Mohamed Elmaouloud Ramamane alisema makubaliano
yamefikiwa kati yao na Jeshi la Afrika la Urusi kwa "lengo la kuhakikisha
wanaondoka salama katika eneo hilo."
Kundi hilo linasema limechukua udhibiti wa mji huo, ambao ulikuwa makao
makuu yasiyo rasmi ya harakati ya kujitenga kwa zaidi ya muongo mmoja kabla ya
kutekwa na jeshi la Mali kwa msaada wa mamluki wa Urusi mwishoni mwa mwaka
2023.
Ingawa Jeshi la Afrika la Urusi limethibitisha kujiondoa Kidal, limesema
shughuli zao zitaendelea kwingineko.
Wapiganaji wengi wa Kikosi cha Urusi Afrika walikuwa wa kundi la mamluki
wa Urusi la Wagner. Kufuatia kifo cha kiongozi wao Yevgeni Prigozhin 2023,
shughuli nyingi za kundi hilo zilichukuliwa na wizara ya ulinzi ya Urusi,
ambayo iliunda Kikosi kipya cha Afrika.
Kikosi cha Afrika kinasimamiwa na Naibu Waziri wa Ulinzi wa Urusi
Yunus-Bek Yevkurov, huku shughuli zake zikiendeshwa na Meja Jenerali Andrey
Averyanov, mtu muhimu katika shirika la ujasusi wa kijeshi la GRU.
Jukumu la Urusi ni kuzisaidia serikali kubaki madarakani, hilo huenda
sanjari na kupata rasilimali muhimu za asili, kama vile dhahabu, almasi na
urani.
Kama Wagner, kikosi cha Afrika kimeshutumiwa kufanya ukatili dhidi ya
raia.
Nchini Mali, wanachama wa Africa Corps wanaripotiwa kulipwa $3,000
(£2,200) kwa mwezi.