Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Trump asema 'hatavumilia ucheleweshaji wowote' kutoka kwa Hamas kuhusu makubaliano ya amani na Israel

Maoni ya rais wa Marekani yanawadia baada ya mashambulizi matatu ya Israel huko Gaza wakati wa mapema huku Hamas ikitaka mazungumzo zaidi.

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya leo. Kwaheri.

  2. Trump asema 'hatavumilia ucheleweshaji wowote' kutoka kwa Hamas kuhusu makubaliano ya amani na Israel

    Rais wa Marekani Donald Trump amezungumzia hatua ya kusuasua ya Hamas na kutoa onyo ya kufuta kila kitu iwapo wataendelea kujikokota.

    "Ninashukuru kwamba Israel imesimamisha kwa muda mashambulizi ya mabomu ili kutoa nafasi ya kuachiliwa kwa mateka na Mpango wa Amani kukamilishwa," amesema kwenye chapisho katika jukwaa lake la Truth Social platform.

    "Hamas lazima ichukue hatua kwa haraka, la sivyo kila kitu kifutwe," ameongeza.

    "Sitavumilia ucheleweshaji wowote, jambo ambalo wengi wanadhani litatokea, au matokeo yoyote ambapo Gaza itajitokeza kuwa tishio tena," ameendelea. "Tumalize hili, HARAKA."

    Ameongeza: "Kila mtu atatendewa haki!"

    Matamshi ya rais yanafuatia mashambulizi matatu tofauti ya anga asubuhi ya leo kwenye Jiji la Gaza, ambapo moja liliua mtu mmoja na kuwaacha wengine kadhaa kujeruhiwa, kulingana na vyanzo vya matibabu katika hospitali ya al-Shifa.

    Soma zaidi:

  3. Viongozi mbalimbali duniani wakaribisha uamuzi wa Hamas

    Afrika Kusini inakaribisha tangazo la Hamas kuwaachilia mateka

    Afrika Kusini "inakaribisha uamuzi wa Hamas wa kuwaachilia mateka wote wa Israel na utayari wake ulioelezwa kwa ajili ya mazungumzo zaidi," kulingana na taarifa kutoka Idara ya Mahusiano ya Ndani.

    Taarifa hiyo inaongeza kuwa ni lazima "mwitikio huo uwe sawa kwa pande zote mbili" yaani Israel.

    Kwa muktadha: Mnamo Desemba 2023, Afrika Kusini iliwasilisha kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ikidai kuwa Israel inajihusisha na "vitendo vya mauaji ya kimbari" huko Gaza. Siku mbili za kusikilizwa kwa kesi zilifanyika mwaka jana huko The Hague, na ICJ ilitoa madai kadhaa kwa Israeli. Mwezi uliopita, na tofauti na kesi ya Afrika Kusini, tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa ilibaini kuwa Israel imefanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza. Israeli daima imekanusha vikali shutuma hizo.

    Hamas iko tayari kwa amani, asema rais wa Uturuki

    Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesisitiza tangazo la Hamas kwamba imekubali sehemu ya mpango wa amani wa Rais Trump.

    "Tunakaribisha" mpango wa rais wa Marekani, ameambia umati katika sherehe mjini Istanbul. Erdogan anaunga mkono Trump, akisema kuwa jibu la Hamas limeonyesha kuwa "iko tayari kwa amani".

    "Fursa" imejitokeza ya kupatikana kwa amani ya kudumu katika kanda, aliongeza.

    Erdogan ametoa wito kwa Israel kusitisha operesheni zake za kijeshi huko Gaza na pande zote zinazohusika katika mzozo huo kuchukua hatua kwa "hisia ya kuwajibika" ili kuleta amani haraka iwezekanavyo.

    Mamlaka ya Palestina yakaribisha 'taarifa chanya' kutoka Hamas

    Hussein al-Sheikh, makamu wa rais wa Mamlaka ya Palestina, amesema anakaribisha "tangazo la Trump la kusitishwa kwa vita, na kauli chanya za Hamas".

    Katika chapisho kwenye X, pia amesema Mamlaka ya Palestina iko tayari kutoa ushirikiano kuelekea usitishaji mapigano, kuachiliwa kwa mateka na wafungwa, kuingia kwa misaada ya kibinadamu huko Gaza, "kujiondoa kamili kwa Israeli kutoka Ukanda wa Gaza, hadi kufikia kipindi cha mpito kuelekea njia ya kisiasa kwa msingi wa suluhisho la serikali mbili".

    Bado kuna njia ya kufuata, ingawa, kabla ya yoyote au yote haya kutokea, kwa sababu wakati Hamas imesema inakubaliana na mpango wa amani, kundi hilo linataka mabadiliko na masharti fulani kutekelezwa.

    Usitishaji vita unaweza kufikiwa, asema mkuu wa EU

    Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen anasema jibu la Hamas kwa pendekezo la mpango wa amani wa Rais Trump ni "la kutia moyo" na kwamba "wakati huu lazima uenziwe".

    "Kusitishwa kwa mapigano mara moja huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka wote kunaweza kufikiwa," rais wa Tume ya Ulaya anachapisha ujumbe huo kwenye mtandao wa X.

    Ameongeza kuwa Ulaya itaunga mkono juhudi zote za kumaliza vita na kupatikana kwa suluhisho la serikali mbili, ambayo anaiita "suluhisho pekee linalowezekana kwa upatikanaji wa amani".

    Soma zaidi:

  4. Mazungumzo ya amani kuanza tena nchini Misri

    Mazungumzo ya makubaliano kati ya Israel na Hamas yanatarajiwa kurejelewa nchini Misri katika siku zijazo, baada ya kundi hilo kukubali kuwaachilia mateka wote waliosalia, lakini limesema linataka mazungumzo zaidi kuhusu masuala mengine.

    Hamas ilikuwa chini ya shinikizo kubwa la kukubali angalau baadhi ya vipengele vya mpango wa Trump kwa Gaza, na hivi ndivyo walivyofanya.

    Lakini mambo muhimu bado hayajaafikiwa, ikiwa ni pamoja na kundi hilo kuachana na silaha, sharti ili wanajeshi wa Israel waondoke Gaza na hakikisho la kwamba Israel haitaanzisha tena vita baada ya mateka kuachiliwa.

    Katika mji wa Gaza, kumekuwa na mashambulizi ya anga licha ya wito wa Trump kwa Israel wa kusitisha mapigano katika eneo hilo.

    Rais Trump amehusika kibinafsi katika mazungumzo hayo, na anatoa shinikizo kwa vita hivyo kumalizika. Hatua kubwa imepigwa katika mpango wa Trump - lakini hii sio hakikisho kwamba makubaliano yamefikiwa.

    Soma zaidi:

  5. Mutharika wa Malawi aapishwa kwa muhula wa pili kama rais

    Peter Mutharika wa Malawi ameapa kumaliza ufisadi serikalini na kujenga upya uchumi uliodorora baada ya kuapishwa Jumamosi kwa muhula wa pili kama rais wa taifa hilo la kusini mwa Afrika.

    Mutharika, 85, alipata zaidi ya 56% ya kura mwezi uliopita, na kumshinda rais anayemaliza muda wake Lazarus Chakwera, 70, aliyepata 33% ya kura zilizopigwa.

    Wapiga kura walimkataa Chakwera baada ya miaka mitano ya mgogoro wa kiuchumi unaozidi kuwa mbaya katika mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani.

    Katika hotuba yake ya kuapishwa, alisema utawala wake unarithi nchi iliyo katika msukosuko wa kiuchumi.

    Malawi inakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, gharama ya juu ya maisha, na ukosefu wa fedha za kigeni ambao umedumaza biashara na kusababisha uhaba wa mafuta, alisema.

    "Hakuna pesa serikalini. Kukopa ni kiwango cha juu sana, na hakuna anayejua pesa zilizokopwa zimeenda wapi," alisema.

    Lakini aliahidi maboresho, akisema: "Tutaiweka sawa nchi hii.

  6. Takriban watu 30 wajeruhiwa katika shambulizi la Urusi kwenye kituo cha reli, Zelensky asema

    Takriban watu 30 wamejeruhiwa kufuatia shambulizi la ndege zisizo na rubani za Urusi kwenye kituo cha reli kaskazini-mashariki mwa Ukraine, Rais wa Ukraine Volodymy Zelensky amesema.

    Katika chapisho kwenye mtandao wa X, alisema kuwa ripoti za awali zilionyesha wafanyakazi wa treni na abiria walikuwa kwenye eneo la tukio katika jiji la Shostka, eneo la Sumy.

    Huduma za dharura zinatolewa katika eneo la tukio na kusaidia watu, alisema na kuongeza kuwa taarifa kuhusu majeruhi bado zinakusanywa.

    Pia alichapisha video inayoonyesha behewa la treni lililoharibika likiwaka moto.

    Soma zaidi:

  7. Takriban watu 66 wauawa Gaza katika saa 24 zilizopita - Hamas

    Wizara ya Afya ya Palestina - Gaza inasema takriban watu 66 wameuawa na uvamizi wa Israel katika saa 24 zilizopita, na kuongeza idadi ya waliouawa katika Ukanda huo tangu 7 Oktoba hadi 67,074.

    Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas inasema watu wengine 265 waliojeruhiwa wamefika katika hospitali za Ukanda wa Gaza katika muda huo huo.

    Wizara hiyo inasema imekuwa vigumu kufikia watu ambao wamenaswa chini ya vifusi.

    Ni nini kimekuwa kimetokea Gaza leo?

    Milipuko kadhaa imeshuhudiwa huko Gaza mapema Jumamosi, huku mji wa Gaza ukikumbwa na mashambulio matatu tofauti ya anga, na kuua mtu mmoja, saa chache baada ya Trump kuitaka Israeli kuacha kushambulia Ukanda huo.

    IDF imewaonya Wapalestina kwamba kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na karibu na Mji wa Gaza bado ni "eneo hatari la mapigano", na kuwataka tena watu kuhamia kusini.

    Viongozi wa upinzani wameunga mkono mpango wa amani wa Trump na kumtaka Netanyahu kuunga mkono mpango huo.

  8. Mashambulizi matatu tofauti ya anga yashambulia Gaza asubuhi ya leo

    Mji wa Gaza umekumbwa na mashambulio matatu tofauti ya anga tangu saa za asubuhi, moja likiwa limeua mtu mmoja na kuwaacha wengine kadhaa kujeruhiwa, kwa mujibu wa vyanzo vya matibabu katika hospitali ya al-Shifa.

    Shambulizi la kwanza lililenga kundi la wakaazi karibu na Shule ya al-Nasr mtaani al-Nasr walipokuwa wakijaribu kuangalia nyumba zao. Lilitekelezwa na helikopta ya Israeli.

    Shamblizi la pili lilishambulia Mtaa wa al-Jalaa, kati ya maeneo ya Zaharna na Ghafri, ingawa hakuna majeruhi walioripotiwa. Shambulizi la tatu la anga lilifanywa na ndege za kivita za Israel karibu na mzunguko wa Hamid, kwenye makutano ya barabara ya al-Nasr.

    Maelezo ya majeruhi au uharibifu bado hayajawekwa wazi.

    Wakati huo huo, magari na ndege zisizo na rubani za Israel (quadcopters) zimeendelea kurusha makombora na kushambulia majengo katika maeneo ambayo jeshi linafanya kazi.

    Soma zaidi:

  9. Sanae Takaichi atarajiwa kuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke wa Japan

    Chama tawala cha kihafidhina nchini Japan kimemchagua Sanae Takaichi kuwa kiongozi wake mpya, na kumuweka katika nafasi ya waziri mkuu wa kwanza mwanamke wa Japan.

    Takaichi ni miongoni mwa wagombea wahafidhina wanaoegemea kwenye haki ya chama tawala. Waziri wa zamani wa serikali, mtangazaji wa TV na mpiga ngoma maarufu, ni mmoja wa watu mashuhuri sana katika siasa za Japani - aliyekuwa na utata wakati huo.

    Anakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na uchumi uliodorora na kaya zinazotatizika na mfumuko wa bei usiokoma na mishahara iliyodumaa.

    Pia atalazimika kuangazia uhusiano unaotetereka kati ya Marekani na Japan na kupitia mpango wa ushuru na utawala wa Trump uliokubaliwa na serikali iliyopita.

  10. Sean 'Diddy' Combs ahukumiwa kifungo cha zaidi ya miaka minne jela

    Mwanamuziki wa muziki wa hip-hop Sean "Diddy" Combs alihukumiwa kifungo cha zaidi ya miaka minne jela siku ya Ijumaa baada ya kukutwa na hatia kwa makosa yanayohusiana na ukahaba yanayowahusisha wapenzi wake wawili wa zamani.

    Mawakili wa Combs walihoji hukumu aliyopewa mteja wao ya miezi 14, wakisema amebadilika baada ya kutumikia miezi 13 katika jela ya New York, lakini waendesha mashitaka walitaka ahukumiwe miaka 11, wakitaja historia yake ya unyanyasaji wa nyumbani.

    Mbali na waendesha mashitaka kuelezea unyanyasaji wa Combs, mahakama ilisikiliza kutoka kwa watoto kadhaa wa Combs, wengine wakilia wazi wazi; mawakili wa utetezi wakimwita mwenye msukumo; na hatimaye, Combs kuomba msamaha mwenyewe.

    Mwishowe, Jaji Arun Subramanian alisema hukumu ilihitajika kuzuia mambo kama hayo, na kutuma ujumbe fulani kwa jamii.

    Kabla ya hakimu kutoa hukumu ya miezi 50, Combs alihutubia mahakama - maneno yake ya kwanza hadharani tangu kesi hiyo ilipoanza.

    Combs aliomba msamaha kwa waathiriwa wake, akiwataja haswa marafiki zake wawili wa kike wa zamani, Casandra Ventura, na "Jane", ambao walitoa ushahidi kwa kutumia jina bandia.

    "Matendo yangu yalikuwa ya kuchukiza, ya aibu, na mabaya," alisema. "Nilipotea sana, nilipotea katika kiburi change."

    Aliendelea kuomba msamaha kwa mama yake na watoto wake.

    "Pole sana. Walistahili yenye ubora," alisema, akimaanisha watoto wake saba, ambao wengi wao walikuwa kwenye chumba cha mahakama.

    Kisha akamwomba hakimu apewe nafasi nyingine, akisema hatahatarisha tena muda wa familia yake. "Mheshimiwa, naomba huruma yako. Naomba huruma yako," Combs alisema.

    "Sina mtu wa kumlaumu ila mimi mwenyewe. Najua kwamba nimejifunza."

    Soma zaidi:

  11. Wakazi wa Gaza bado wako katika "hali mbaya" – Shirika la MSF

    Mratibu wa huduma za dharura huko Gaza wa shirika la Médecins Sans Frontières (MSF), ameiambia BBC kwamba watu katika Jiji la Gaza wanaishi katika "hali mbaya" huku kukiwa na upungufu wa chakula, maji na huduma za afya.

    MSF imelazimika kusitisha "shughuli muhimu za matibabu" katika jiji la Gaza mwishoni mwa Septemba, ambayo Granger anasema ilitokana na kuzorota kwa hali ya usalama na kuongezeka kwa mashambulizi ya anga.

    Mfanyikazi wa MSF Omar Hayek aliuawa huko Gaza siku ya Alhamisi, mwanachama wa 14 wa MSF kuuawa huko Gaza tangu 7 Oktoba 2023.

    "Hili ni jukumu kutoka kwa mamlaka ya Israeli, unapaswa kulinda misheni ya kibinadamu," Granger anasema, akielezea "siku ngumu" kufuatia kifo cha mwenzake.

    "Wahudumu wa misaada ya kibinadamu hawajalindwa, fikiria hali ikoje kwa raia wengine wote."

    Na wenyeji wanatamani sana kujua ikiwa hatua za hivi punde za kisiasa zinamaanisha mwisho wa vita.

    Soma zaidi:

  12. Netanyahu ajibu Hamas akiadhidi kushirikiana na Trump

    Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imetoa taarifa ya mistari miwili, ikisema kuwa nchi hiyo itashirikiana na Marekani kuhusu "mpango wa Trump" wa amani.

    "Kwa kuzingatia majibu ya Hamas, Israel inajiandaa kutekeleza mara moja awamu ya kwanza ya mpango wa Trump wa kuachiliwa mara moja kwa mateka wote," Netanyahu alisema katika taarifa yake iliyotafsiriwa kutoka Kiebrania.

    "Tutaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano kamili na Rais na timu yake ili kumaliza vita kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa na Israel ambazo zinaendana na maono ya Rais Trump."

    Pia unaweza kusoma:

  13. Trump asema Hamas iko 'tayari kwa amani ya kudumu'

    Rais wa Marekani Donald Trump ametoa taarifa kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social unaoonyesha kuwa Hamas imekubali mpango wa amani.

    Ujumbe wa Trump unasema: "Kulingana na Taarifa iliyotolewa hivi punde na Hamas, ninaamini wako tayari kwa AMANI ya kudumu. Israel lazima isitishe mara moja mashambulizi ya mabomu huko Gaza, ili tuweze kupata mateka kwa usalama na haraka!

    "Kwa sasa, ni hatari sana kufanya hivyo. Tayari tuko kwenye majadiliano kuhusu maelezo yatakayofanyiwa kazi. Hili halihusu Gaza pekee, hili ni kuhusu AMANI iliyotafutwa kwa muda mrefu katika Mashariki ya Kati."

    Hamas wamesema nini?

    Katika taarifa yake ikijibu pendekezo la amani la Marekani, Hamas inasema inakubali "kuwaachilia wafungwa wote wa Israel, walio hai na waliokufa, kwa mujibu wa mpango wa mabadilishano uliopendekezwa na Rais Trump, mradi masharti ya ubadilishanaji yametimizwa".

    Taarifa hiyo inaongeza kuwa "inafanya upya makubaliano yake ya kukabidhi utawala wa Ukanda wa Gaza kwa chombo huru cha Wapalestina" kwa kuzingatia "makubaliano ya kitaifa ya Palestina na uungaji mkono wa nchi za Kiarabu na Kiislamu".

    Juu ya mustakabali wa Gaza na haki za watu wa Palestina, Hamas inasema hii "inahusishwa na msimamo wa kitaifa unaozingatia sheria na maazimio husika ya kimataifa, na inajadiliwa ndani ya mfumo wa kitaifa" ambao itakuwa sehemu yake.

    Soma zaidi:

  14. Hujambo msomaji wetu. Karibu katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 04/10/2025. Mimi ni nahodha wako Asha Juma.