Moja kwa moja, Trump atishia kutangaza Mlango Bahari wa Hormuz kuwa eneo la Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump, amesema hivi karibuni atatangaza Mlango Bahari wa Hormuz kuwa sehemu ya eneo la Marekani, akidai kuwa Iran imeathirika vibaya na vita vilivyotokea eneo hilo.

Muhtasari

Trump atishia kutangaza Mlango Bahari wa Hormuz kuwa eneo la Marekani

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Arsenal wanalenga kuanza msimu kwa ushindi mkubwa

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Arsenal wataanza msimu mpya wakiwa na azma ya kuonyesha mapema kuwa wana uwezo wa kushindania mataji, baada ya msimu uliopita wenye matokeo mchanganyiko na changamoto kadhaa, huku shughuli zao kwenye soko la uhamisho zikianza kwa utulivu.

    Kikosi cha Mikel Arteta kilianza maandalizi ya msimu kwa ushindi mzuri dhidi ya MK Dons na Girona, kabla ya kupata vipigo kutoka kwa Real Betis na Borussia Dortmund. Arsenal walihitimisha maandalizi yao kwa sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Como ya Serie A nchini Italia.

    Nje ya uwanja, Arsenal wamekuwa na utulivu katika kipindi hiki cha kiangazi, huku usajili wa Bruno Guimaraes ukiwapa nguvu zaidi baada ya kuimarisha safu yao ya kiungo.

    Iwapo Arsenal wataifunga Manchester City, ambayo inaanza enzi mpya baada ya kuondoka kwa Pep Guardiola, ushindi huo utakuwa ujumbe kwamba bado ni moja ya timu zinazopaswa kuogopwa na wapinzani wao katika mbio za ubingwa.

    Arsenal wataingia msimu huu wakilenga kutetea taji lao, huku ushindi dhidi ya Manchester City ukiweza kuwa mwanzo muhimu wa safari hiyo.

    Soma Zaidi:

  2. Meli ya kivita ya Marekani yaelekea Mashariki ya Kati kuchukua nafasi ya USS Abraham Lincoln

    Picha ya meli ya USS George Washington

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Picha ya meli ya USS George Washington

    Meli ya kubeba ndege za kivita ya Marekani imeanza safari kuelekea Mashariki ya Kati kuchukua nafasi ya meli ya USS Abraham Lincoln, ambayo maelfu ya mabaharia wake wameripotiwa kukabiliwa na uhaba wa chakula na mazingira magumu ya maisha wakati wa operesheni yake ya miezi tisa.

    Kulingana na uchunguzi wa BBC, meli ya USS George Washington, iliyokuwa karibu na Malaysia siku ya Alhamisi, huenda ikafika katika eneo hilo ndani ya takriban siku tisa.

    Familia za baadhi ya mabaharia wa USS Abraham Lincoln zimeelezea wasiwasi kuhusu kudorora kwa afya ya akili ya jamaa zao kutokana na hali ngumu wanayokabiliana nayo, huku kukiwa na ripoti za baadhi ya mabaharia wakitaka kujirusha ndani ya bahari.

    Jeshi la Wanamaji la Marekani limekubali kuwepo kwa matatizo ya usambazaji wa mahitaji muhimu kwa wanajeshi hao, lakini limekanusha kuwa wanajeshi hao wanakabiliwa na changamoto za afya ya kiakili.

    USS Abraham Lincoln, ina takriban wanajeshi 5,000.

    Akizungumza na waandishi wa habari hapo jana, Rais wa Marekani Donald Trump alipuuzilia wasiwasi ambao umetolewa na familia za wanajeshi walioko katik meli hiyo ambao wanadai muda wa oparesheni ya meli hiyo imekuwa ndefu sana.

    Soma pia:

  3. Watu wanne wauawa katika shambulizi la makombora la Wahouthi nchini Yemen

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Serikali ya Yemen imewalaumu kundi la wapiganaji la Wahouthi kwa kurusha makombora sita ya kibalistiki katika bandari ya Mocha, kwenye Bahari ya Shamu, hapo jana na kuwaua watu wanne.

    Kulingana na maafisa wa serikali ya Yemen, shambulizi hilo lililenga miundombinu ya kiraia na maeneo ya bandari, huku boti kadhaa za uvuvi zikichomwa moto.

    Kwa upande mwingine, Wahouthi wamesema katika taarifa yao kuwa walilenga vituo vya kijeshi, silaha na ndege za vikosi vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia huko Mocha, kwa kuwarushia makombora.

    Tukio hili limetokea wakati mvutano unaendelea kutokota eneo hilo kati ya Wahouthi na Saudi Arabia, Pamoja na mvutano kati ya Marekani na Iran.

    Soma pia:

  4. 'Mlango Bahari wa Hormuz ulikuwa na utaendelea kuwa wa Iran' - Kazem

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Akijibu kauli ya Rais wa Marekani Donald Trump ya kutangaza Mlango wa Bahari wa Hormuz kuwa eneo la Marekani, Naibu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Kazem Gharibabadi, amesema kuwa “Mlango wa Bahari wa Hormuz ulikuwa wa Iran, ni wa Iran, na utaendelea kuwa wa Iran.”

    Kazem Gharibabadi alichapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X na kusisitiza kuwa “Mlango wa Bahari wa Hormuz hauwezi kutekwa kupitia ujumbe uliochapishwa kwenye X au meli ya kubeba ndege za kivita.”

    Waziri huyo aliongezea kuwa Iran “haiogopi vitisho wala maonyesho ya nguvu.”

    Gharibabadi pia alidai kwamba “Marekani hadi sasa imepata kushindwa katika mikakati yake ya vita.”

    Kulingana naye, “Iran pekee ndiyo yenye mamlaka ya kufunga au kufungua Mlango wa Bahari wa Hormuz.”

    Soma pia:

  5. Trump atishia kutangaza Mlango Bahari wa Hormuz kuwa eneo la Marekani

    Picha ya Donald Trump

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Picha ya Donald Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwamba hivi karibuni atatangaza Mlango Bahari wa Hormuz kuwa sehemu ya eneo la Marekani, akidai kuwa Iran imeathirika vibaya na vita vilivyotokea eneo hilo.

    “Baada ya kuishinda Iran, ambayo sasa imeathirika vibaya,hivi karibuni nitatangaza Mlango Bahari wa Hormuz kuwa eneo la Marekani,” Trump alisema katika mkutano wa kisiasa mjini New York.

    Kauli ya Trump imekuja wakati mkwamo unashuhudiwa kati ya Washington na Tehran kuhusu mlango huo wa bahari.

    Mlango Bahari wa Hormuz ni njia muhimu ambayo hupitisha kiasi kikubwa cha mafuta na bidhaa tofauti duniani.

    Iran imeweka udhibiti katika sehemu kubwa ya mlango huo, na kuzuia meli nyingi za mizigo za kiraia kupita, huku Jeshi la Wanamaji la Marekani likiweka kizuizi katika bandari za Iran katika jaribio la kudhoofisha uchumi wa nchi hiyo.

    “Tumeweka kizuizi. Hakuna meli itakayopita isipokuwa sisi wenyewe tutake ipite,” Trump aliwaambia wafuasi wake.

    Naibu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Kazem Gharibabadi, amejibu kauli ya Trump mapema hii leo kupitia mtandao wa X na kusema,

    “Mlango huu wa bahari hautafunguliwa wala kufungwa isipokuwa kwa amri ya Iran, na msipo kubali ukweli kuwa mmeshindwa, mtaendelea kujidanganya, na Iran itaendelea kuweka kizuizi.”

    Gharibabadi alisisitiza kuwa Mlango wa Bahari wa Hormuz utaendelea kumilikiwa na Iran, “Mlango Bahari wa Hormuz ulikuwa wa Iran, ni wa Iran, na utaendelea kuwa wa Iran.”

    Soma pia:

  6. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja