Twiga Stars yaandika historia kwa kuifunga Afrika Kusini WAFCON 2026

Chanzo cha picha, CECAFA
Tanzania imeandika historia kwa kupata ushindi wake wa kwanza kabisa katika Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) baada ya kuifunga mabingwa wa mwaka 2022, Afrika Kusini, mabao 2 kwa 1 katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi B.
Twiga Stars ilitoa moja ya matokeo ya kushangaza zaidi katika mashindano hayo baada ya kuonyesha mchezo wa nidhamu na ujasiri dhidi ya Banyana Banyana, huku Hasnath Ubamba akifunga bao la ushindi dakika ya 87.
Diana Msewa aliitanguliza Tanzania mbele dakika ya 37 baada ya Twiga Stars kuanza mchezo kwa kasi na kulisukuma lango la Afrika Kusini mara kwa mara.
Hata hivyo, Bambanani Mbane aliisawazishia Afrika Kusini katika muda wa nyongeza wa kipindi cha kwanza, na kuifanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa sare ya bao 1 kwa 1.
Kipindi cha pili kilikuwa na ushindani mkubwa huku Afrika Kusini ikitafuta bao la ushindi, lakini Twiga Stars iliendelea kujilinda kwa umakini na kutumia mashambulizi ya kushtukiza.
Dakika ya 87, Hasnath Ubamba aliyeingia akitokea benchi aliifungia Tanzania bao la ushindi, lililozua shangwe kubwa miongoni mwa wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki.
Ushindi huo ni hatua muhimu kwa soka la wanawake Tanzania. Kabla ya mchezo huo, Twiga Stars ilikuwa imecheza mechi sita za WAFCON bila kushinda, ikipata sare moja na kupoteza tano.
Matokeo hayo pia yanaongeza matumaini ya Tanzania kutinga hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano hayo.
Kwa upande wa Afrika Kusini, mabingwa wa mwaka 2022 wameanza vibaya kampeni yao ya kutwaa ubingwa kwa mara nyingine, na sasa watakuwa chini ya shinikizo la kupata matokeo mazuri katika mechi zao zilizosalia za Kundi B ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua inayofuata.
Kwa Twiga Stars, ushindi huo dhidi ya moja ya timu zenye nguvu zaidi barani Afrika unaweza kuwa chachu ya kujiamini katika harakati za kuandika historia nyingine kwenye WAFCON 2026.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania, Twiga Stars, kwa kuanza vyema michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 nchini Morocco.
“Ninaungana na Watanzania wote kuitakia kila la kheri Twiga Stars inapoendelea kupeperusha bendera ya Taifa letu katika michezo inayofuata. Endeleeni kupambana kwa moyo huo huo, mkionyesha uzalendo, nidhamu na ari ya ushindani inayolitangaza vyema Taifa letu,” amesema Rais Samia Suluhu Hassan.
Fuatilia hapa:

Chanzo cha picha, cecafa























