Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump atangaza Mlango Bahari wa Hormuz kuwa eneo la Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwa sasa Mlango Bahari wa Hormuz ni eneo la Marekani na Iran inaonekana haipo tayari kufikia makubaliano.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Tazama kwa picha uzinduzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Julius Nyerere

    Uzinduzi wa bwawa kubwa zaidi Afrika Mashariki ka kuzalisha umeme umefanyika hii leo.

    Bwawa hilo lililopewa jina la Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, lina uwezo wa kuzalisha megawatt 2115 za umeme, hivyo kuwa moja ya mabwawa makubwa ya kufua umeme barani Afrika.

    Tazama kwa picha uzinduzi wa bwawa hilo:

  2. Bingwa wa zamani wa dunia wa bondia Zolani Tete, auawa kwa kupigwa risasi Afrika Kusini

    Bingwa wa zamani wa dunia wa bondia, Zolani “Last Born” Tete amepigwa risasi na kuuawa nje ya nyumba yake katika mkoa wa Eastern Cape nchini Afrika Kusini hapo jana, polisi na Waziri wa Michezo wa nchi hiyo wametoa taarifa.

    Tete, mwenye umri wa miaka 38, alikuwa akielekea nyumbani kwake katika mji wa Mdantsane wakati wanaume wawili waliokuwa na silaha na waliovaa barakoa waliposhuka kutoka kwenye gari na kuanza kumfyatulia risasi.

    Kuuawa kwa Tete kunaamsha tena mjadala kuhusu uhalifu wa kimabavu Afrika Kusini. Taifa hilo linaendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu zaidi vya mauaji duniani licha ya kupungua kwa idadi ya mauaji katika kipindi cha hivi karibuni.

    Kifo cha bingwa huyo wa bondia duniani pia kimewagusa sana wakazi wa Mdantsane, mji wa Eastern Cape, mji ambao umezalisha baadhi ya mabondia waliofanikiwa zaidi nchini Afrika Kusini.

    Mwanamke mwenye umri wa miaka 27 aliyekuwa akisafiri pamoja na Tete alipigwa risasi mara kadhaa na kukimbizwa hospitalini.

    Polisi wameanza uchunguzi, huku chanzo na sababu ya bondia huyo kushambuliwa bado haijajulikani.

    Tete alitwaa taji la dunia la IBF katika uzani wa junior-bantamweight mwaka 2014 baada ya kumshinda Mjapani Teiru Kinoshita mjini Kobe, Japan. Baadaye alitwaa pia taji la WBO katika uzani wa bantamweight.

    Kimataifa, Tete anakumbukwa zaidi kwa kumpiga ndani ya sekunde 11 raia mwenzake wa Afrika Kusini, Siboniso Gonya, mjini Belfast, Ireland Kaskazini, mwezi Novemba 2017.

    Ushindi huo uliweka rekodi ya kumalizika kwa haraka zaidi pambano la kuwania taji la dunia.

    Soma pia:

  3. Tanzania yazindua rasmi bwawa la umeme

    Na Florian Kaijage

    Bwawa kubwa zaidi Afrika Mashariki la kufua umeme wa nguvu za maji unazinduliwa leo nchini Tanzania.

    Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ndiye mgeni rasmi katika uzinduzi huo. Waziri Mkuu wa Misri, Mostafa Madbouly anamwakilisha Rais, Abdel Fattah el Sisi wa Misri, anakotokea mkandarasi mkuu wa mradi huo, kampuni ya Arab Contractors.

    Bwawa hilo lililopewa jina la Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, lina uwezo wa kuzalisha megawatt 2115 za umeme, hivyo kuwa moja ya mabwawa makubwa ya kufua umeme barani Afrika.

    Mradi huo ulianza kutekelezwa Juni, 2019 baada ya mkataba kusainiwa mwaka 2018 wakati wa uongozi wa Rais John Magufuli aliyehuisha wazo na usanifu wa bwawa hilo la mwanzoni mwa miaka ya 1970, lakini utekelezaji wake ulishindikana kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa fedha na pingamizi kutoka kwa watetezi wa hifadhi ya mazingira, waliopinga ukataji wa miti kupisha ujenzi huo

    Bwawa la Mwalimu Nyerere lipo ndani ya iliyokuwa mbuga ya wanyama ya Selous, iliyopo kwenye orodha ya maeneo ya urithi wa dunia chini ya Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO).

    Ujenzi wake pamoja na mitambo ya kufua umeme umegharimu dola za Marekani bilioni 2.9. Lipo pembezoni mwa mto Rufiji.

    Soma pia:

  4. Tanzania yaanza mchakato wa kuwarejesha raia wake nyumbani kutoka Afrika Kusini

    Tanzania itaanza kuwarejesha kwa hiari raia wake wanaoishi katika mkoa wa KwaZulu-Natal, Afrika Kusini, kuanzia tarehe 26 mwezi Agosti.

    Kundi la kwanza litarejea nchini Tanzania, kupitia ndege ya Air Tanzania, kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa King Shaka ulioko mjini Durban.

    Ubalozi wa Tanzania ulioko mjini Pretoria, umesema kuwa Watanzania waliosajiliwa haswa wanaoishi mjini Durban, watapitia mchakato wa kupewa vibali vya kurejea Tanzania kwa hiari, tarehe 25 na 26 mwezi huu wa Agosti.

    Zoezi hilo litawahusisha Watanzania wasio na pasipoti, ambao muda wa kutumika wa pasipoti zao umekwisha au kupotea, pamoja na watoto waliozaliwa Afrika Kusini.

    Watanzania wasio na pasipoti watapewa hati za dharura za kusafiria ili kuwawezesha kurejea nchini humo.

    Uamuzi wa kuwarejesha Watanzania nchini unakuja wakati kumekuwa na maandamano ya kupinga wahamiaji nchini Afrika Kusini.

    Mataifa kadhaa ya Afrika tayari yamewaondoa raia wao nchini humo.

    Soma pia:

  5. Zaidi ya wanajeshi 750 wa Marekani wamejeruhiwa katika vita vya Iran

    Gazeti la Washington Post limeripoti kuwa idadi ya wanajeshi wa Marekani waliouawa au kujeruhiwa katika vita vya Iran imefikia 774, baada ya wizara ya ulinzi kuongeza idadi ya wanajeshi waliojeruhiwa hivi karibuni.

    Kulingana na mfumo wa wizara ya ulinzi wa kurekodi majeruhi, kufikia sasa wanajeshi 18 wa Marekani wameuawa na wengine 756 kujeruhiwa katika vita vya Iran na Marekani.

    Usitishaji mapigano kati ya Marekani na Iran ulikamilika siku ya Jumatatu na muda huo haujaongezwa, ila hakuna upande ambao umetekeleza oparesheni yoyote kubwa ya kijeshi.

    Soma pia:

  6. Watu 16 wauawa katika shambulio la Urusi nchini Ukraine

    Timu ya waokoaji nchini Ukraine, inaendelea kuwatafuta manusura katika duka moja la jumla lililoshambuliwa na ndege isiyo na rubani ya Urusi.

    Kulingana na maafisa wa polisi, watu 16 wameuawa na wengine 130 kujeruhiwa katika kituo hicho cha kibiashara mjini Kryvyi Rih hapo jana. Watu tisa bado hawajulikani walipo.

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, amesema shambulio hilo “ni la kikatili” kwani lilitekelezwa kwa awamu mbili, awamu ya pili ikiwalenga wahudumu wa dharura waliokuwa wamefika katika eneo la mkasa.

    Wakati huo huo, maafisa wa polisi wa eneo hilo wamesema angalau watu wawili zaidi wameuawa katika mashambulizi mengine ya Urusi yaliyofanyika mapema hii leo. Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema ililenga miundombinu ya uchukuzi na maghala ya Ukraine.

    Mkuu wa utawala wa kijeshi wa eneo la Dnipropetrovsk, Oleksandr Hanzha, amesema watoto 23 ni miongoni mwa waliojeruhiwa katika shambulio la Ijumaa kwenye duka hilo la jumla la kibiashara.

    Soma pia:

  7. Raia 13 wa Tunusia hawajulikani walipo baada ya boti lao kuzama bahari ya Mediterenia

    Takriban raia 13 wa Tunisia, hawajulikani walipo baada ya boti iliyokuwa imebeba wahamiaji kuzama katika pwani ya Tunisia ikiwa inaelekea Italia, huku watu wawili wakiokolewa.

    Akizungumza na shirika la habari la Reuters, Mostafa Abdelkebir, mkuu wa shirika la Tunisian Observatory for Human Rights, alisema boti hiyo iliondoka mapema siku ya Alhamisi.

    Mmoja wa manusura hao wawili aliwaambia waokoaji kuwa walikuwa wamekwama baharini kwa saa kadhaa kabla ya chombo chao kupinduka.

    Tunisia ni mojawapo ya maeneo makuu yanayotumiwa na wahamiaji wanaovuka Bahari ya Mediterania, lakini safari hizo zimepungua kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kutokana na operesheni kali dhidi ya uhamiaji na kuimarishwa kwa usalama wa baharini.

    Njia ya katikati ya Bahari ya Mediterania ni mojawapo ya njia hatari zaidi za uhamiaji duniani, inayotumiwa na wahamiaji kutoka Afrika na Mashariki ya Kati wanaotaka kufika Ulaya, mara nyingi wakitumia boti zisizo salama kwa safari za baharini.

    Soma pia:

  8. Marekani yatangaza ushuru wa 50% kwa bidhaa kutoka Canada

    Marekani imetangaza ushuru wa asilimia 50 kwa baadhi ya bidhaa kutoka Canada, baada ya kushindwa kufikia makubaliano ya kibiashara.

    Ushuru huo, ulioanza kutekelezwa jana usiku, utaathiri bidhaa za Canada zenye thamani ya takribani dola bilioni 20 za Marekani.

    Ushuru huo mpya umeongeza mvutano kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney, na huenda ukalemaza biashara huru kati ya mataifa hayo mawili.

    Carney amesema amesitisha mazungumzo ya kibiashara na Marekani na kwamba Canada italipiza kisasi kwa kuweka ushuru wa thamani sawa, “dola kwa dola,” dhidi ya ushuru huo mpya.

    “Nimeamua kusitisha mazungumzo ya kibiashara na Marekani na nimewaelekeza wajumbe wa Canada wanaoshiriki katika mazungumzo hayo kurejea Ottawa,” alisema Carney.

    Soma pia:

  9. Mlango Bahari wa Hormuz ni eneo la Marekani - Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa Mlango Bahari wa Hormuz ni eneo la Marekani.

    “Kwa sasa natangaza Mlango wa Hormuz kuwa eneo la Marekani.”

    Akifanya kampeni katika jimbo la South Carolina, Trump alisisitiza kuwa hawataruhusu Iran kumiliki silaha za nyuklia.

    Kauli hizo mpya zinakuja wakati Marekani imeongeza shinikizo la kiuchumi dhidi ya Iran katika siku za hivi karibuni, huku ikiendelea kuweka kizuizi cha kijeshi katika eneo hilo la bahari.

    Washington inatarajiwa kutangaza siku ya Jumatatu vikwazo vipya vya kiuchumi dhidi ya Iran. Maafisa wa Marekani wanasema vikwazo hivyo vinaweza pia kuathiri washirika wakuu wa kibiashara wa Iran, ikiwemo China.

    Soma pia:

  10. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja