Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump asema China sasa kununua mafuta Marekani na kutoipatia silaha Iran

Rais Trump amesema mazungumzo ya biashara kati ya Marekani na China “yamekwenda vizuri zaidi kuliko mara ya mwisho”, akieleza kuwa duru hii yalikuwa makubwa zaidi kuliko makubaliano 36 yaliyosainiwa katika mazungumzo yaliyopita.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Mlipuko mpya wa virusi vya Ebola waua watu 65 DRC

    Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola umeripotiwa katika wilaya ya Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Takriban visa 246 na vifo 65 vimeripotiwa, katika miji ya uchimbaji dhahabu ya Mongwalu na Rwampara, hii ni kulingana na taarifa kutoka Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC).

    Ugonjwa wa Ebola uligunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 1976 nchini DRC na inaaminika kuwa ilisambazwa kutoka kwa popo. Huu ni mlipuko wa 17 wa ugonjwa huo hatari nchini humo.

    Ugonjwa huo husambazwa kupitia kugusana wa moja kwa moja, na husababisha kutokwa damu pamoja na kufeli kufanya kazi kwa viungo vya mwili.

    Dalili za ugonjwa huu ni homa, maumivu ya misuli, uchovu, maumivu ya kichwa na koo. Hakuna tiba ya Ebola hadi sasa.

    Unaweza kusoma;

    • Mpelelezi wa virusi ambaye aligundua Ebola mwaka 1976
    • Kwanini waliopona Ebola wanaambiwa waepuke kujamiiana kabla ya siku 90?
  2. Trump na Xi wanakula nini wakati wa chakula cha mchana?

    Rais wa Marekani, Donald Trump na Rais wa China Xi Jinping kwa sasa wanashiriki chakula cha mchana cha kikazi. Kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani, menyu yao inajumuisha:

    • Samaki aina ya kamba iliyokaangwa kwa ukoko mkavu na kwa mtindo wa kuchochewa jikoni.
    • Supu ya dagaa yenye samaki aina ya chewa waliokatwakatwa
    • Minofu ya nyama ya ng’ombe iliyokaangwa na kujazwa uyoga aina ya morel
    • Kuku wa Kung Pao na scallops
    • Mboga za kienyeji zilizochemshwa pamoja na machipukizi ya mianzi, uyoga na maharagwe
    • Nyama ya ng’ombe ya mchuzi ndani ya mkate
    • Andazi iliyotengezwa na nyama ya nguruwe na kamba iliyopikwa kwa mvuke
    • Keki ya chokoleti
    • Matunda na aiskrimu
    • Kahawa au chai

    Wakati huo huo, waandishi wa habari wanaosafiri na msafara wa Ikulu ya Marekani wameagiziwa chakula cha McDonald's na kupelekewa kwenye magari yao.

  3. Waitaliano watano wafariki wakati wa kupiga mbizi kwenye mapango ya kisiwa cha Maldives

    Raia watano wa Italia wamefariki katika ajali ya kupiga mbizi (scuba diving) katika kisiwa cha Maldives, wizara ya mambo ya nje mjini Roma imesema.

    Wizara hiyo imesema waogeleaji hao wanaaminika kufariki wakati wakijaribu kuchunguza mapango katika kina cha mita 50 (futi 164), tukio lililotokea katika eneo la Vaavu Atoll.

    Jeshi la Maldives limesema mwili mmoja umepatikana ndani ya pango lililoko takriban mita 60 chini ya maji, huku waogeleaji wengine wanne wakiaminika bado wako eneo hilo.

    Limesema waokoaji wenye vifaa maalum wametumwa eneo la tukio, likieleza kuwa operesheni ya utafutaji ni ya hatari kubwa sana.

    Tukio hilo linaaminika kuwa ajali mbaya zaidi ya kupiga mbizi kuwahi kutokea katika taifa hilo dogo la Bahari ya Hindi, ambalo ni kivutio kikubwa cha watalii kutokana na visiwa vyake vya matumbawe.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya eneo hilo, Waitaliano hao waliingia majini Alhamisi asubuhi.

    Wafanyakazi wa boti ya kupiga mbizi waliokuwa wakisafiri nao waliripoti kutoweka kwao baada ya kushindwa kurejea juu ya maji kwa wakati uliotarajiwa.

    Polisi walisema hali ya hewa ilikuwa mbaya katika eneo hilo, takriban kilomita 100 kusini mwa mji mkuu Malé, na onyo la njano lilitolewa kwa boti za abiria na wavuvi.

    Unaweza kusoma pia:

  4. FBI yatoa zawadi ya dola 200,000 kumtafuta afisa wa zamani wa ujasusi anayedaiwa kuipeleleza Iran

    Kitengo cha kijasusi cha Marekani cha FBI kimetangaza zawadi ya dola 200,000 kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kumkamata Monica Witt, afisa wa zamani wa ujasusi wa anga na upelelezi wa kijeshi.

    Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi Mei 14, FBI ilieleza kuwa Witt aliwahi kuhudumu katika jeshi la anga la Marekani kati ya mwaka 1997 na 2008, na baadaye kufanya kazi kama mwanakandarasi wa serikali ya Marekani hadi mwaka 2010. Ilisema majukumu yake yalimpa upatikanaji wa taarifa za siri na za juu kabisa kuhusu ujasusi wa kigeni na upelelezi wa kijeshi, ikiwemo utambulisho wa maafisa wa siri wa taasisi za ujasusi za Marekani.

    Kwa mujibu wa FBI, Witt alikimbilia Iran mwaka 2013. Inadaiwa kuwa baadaye alitoa taarifa kwa serikali ya Iran zilizoathiri usalama wa taarifa za siri za ulinzi wa taifa la Marekani na programu zake za kijeshi.

    Aidha, anatuhumiwa kufichua taarifa zilizohatarisha maisha ya wanajeshi wa Marekani walioko nje ya nchi pamoja na familia zao, na pia kuwasaidia Wairani kuwatafuta maafisa wa zamani wa serikali ya Marekani ili washambuliwe.

    FBI imesema kuwa licha ya shtaka dhidi yake, bado hayupo mikononi mwa sheria.

    Mwisho wa taarifa hiyo, FBI imetangaza zawadi hiyo ya dola 200,000 na kuomba ushirikiano wa umma katika kumsaidia kumtafuta na kumkamata afisa huyo wa zamani wa ujasusi.

    Pia unaweza kusoma pia:

  5. Trump: China yataka Mlango wa Hormuz ubaki wazi

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa China inataka Mlango wa bahari wa Hormuz ubaki wazi, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa usafirishaji wa mafuta.

    Aidha amesema China inanunua kiasi kikubwa cha mafuta kupitia eneo hilo, na hivyo inapendelea shughuli hizo ziendelee bila vikwazo.

    Trump ameongeza kuwa Rais wa China Xi Jinping ameonyesha utayari wa kusaidia kufanikisha makubaliano ya kuhakikisha mlango huo unabaki wazi.

    “Yeyote anayenunua kiasi hicho cha mafuta ana uhusiano fulani nao, lakini alisema angependa kusaidia endapo ataweza,” Trump amesema, akisisitiza kuwa China ingependa kuona Mlango wa Hormuz ukiendelea kuwa wazi.

    Pia Trump amemalizia kwa kusema Marekani na China wana mtazamo unaofanana kuhusu suala la Iran.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Bendera ya Israel yapeperushwa katika msikiti wa Al Aqsa

    Waziri wa Usalama wa Kitaifa wa mrengo wa kulia nchini Israel, Itamar Ben-Gvir, amevunja utaratibu wa muda mrefu unaohusu maeneo ya ibada ya dini tofauti katika eneo hilo baada ya kupeperusha bendera ya Israel karibu na Msikiti wa Al Aqsa.

    Video zilizochapishwa zinaonyesha waziri huyo akiinua bendera ya Israel huku wimbo wenye maneno “Msikiti mtukufu wa Al Aqsa uko mikononi mwetu” ukisikika.

    Maelfu ya Waisraeli pia wamefanya maandamano katika eneo hilo wakishiriki tukio la kila mwaka la kidini na kitaifa.

    Maandamano hayo yanayojulikana kama “Flag March” hufanyika kuadhimisha kumbukumbu ya Israel kuteka Jerusalem Mashariki wakati wa vita vya mwaka 1967.

    Mwandishi wa BBC mjini Jerusalem amesema kuwa tukio hilo mara nyingi huambatana na vurugu, misukosuko pamoja na kauli za kibaguzi dhidi ya Wapalestina wanaoishi katika maeneo hayo ya Jerusalem.

    Mwaka huu, makumi ya wanaharakati wa amani kutoka Israel walijaribu kuzuia kile walichokitaja kuwa vitendo vya ukatili vinavyoambatana na maandamano hayo.

    Soma zaidi:

  7. Bei ya mafuta yapanda kwa kiwango cha juu nchini Kenya

    Wakenya wameingiwa na wasiwasi baada ya serikali kuongeza bei ya rejareja ya dizeli kwa Shilingi 46.29 za Kenya kwa lita na petroli kwa Shilingi 16.65 za kenya katika tangazo lililotolea na Mamlaka ya kudhibiti kawi na nishati ya (EPRA).

    Jijini Nairobi, Petroli itauzwa kwa shilingi 214.25 za Kenya, wanaotumia dizeli ikiwalazimu kuinunua kwa shilingi 242.92 za Kenya huku watumiaji wa mafuta ya taa kuipata bidhaa hiyo na shilingi 152.78 za Kenya kwa kila lita kuanzia Alhamisi kwa siku 30 zijazo.

    Kwa mujibu wa wachangunizi wa kiuchumi, ongezeko hilo linatarajiwa kuongeza gharama za utengenezaji na usafirishaji, hali inayoweza kusababisha wawekezaji na wafanyabiashara kuongeza bei za bidhaa kwa wanunuzi.

    Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, EPRA imesema bei ya mafuta ya taa haitabadilika katika kipindi cha bei kitakachoanza leo Mei 15 hadi Juni 14, 2026.

    Hatua hiyo inafuta nafuu iliyoshuhudiwa mwezi uliopita baada ya serikali kupunguza kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kutoka asilimia 13 hadi asilimia 8 kupitia Tangazo la Kisheria Na. 70 la Aprili 15, 2026.

    “Katika kipindi hiki cha tathmini, bei ya juu inayoruhusiwa ya petroli imeongezeka kwa Shilingi 16.65 za Kenya kwa lita na dizeli kwa Shilingi 46.29 za Kenya kwa lita, huku mafuta ya taa yakibaki bila mabadiliko,” EPRA imesema.

    Mamlaka hiyo ilieleza kuwa ongezeko hilo limetokana na kupanda kwa bei za mafuta katika soko la kimataifa pamoja na gharama kubwa za kuagiza mafuta kutoka nje.

    Kwa mujibu wa EPRA, wastani wa gharama ya kuagiza petroli uliongezeka kwa asilimia 10 kutoka dola 823.27 za Marekani kwa mita ya ujazo mwezi Machi 2026 hadi dola 906.23 mwezi Aprili.

    Dizeli ilirekodi ongezeko kubwa zaidi la asilimia 20.32, kutoka dola 1,073.82 hadi dola 1,291.98 kwa mita ya ujazo katika kipindi hicho.

    EPRA ilibainisha kuwa bidhaa za mafuta katika soko la kimataifa huuzwa kwa dola za Marekani, hivyo huathiriwa na mabadiliko ya bei ya mafuta duniani pamoja na viwango vya ubadilishaji fedha za kigeni.

    Bei hizo pia zinajumuisha VAT kwa mujibu wa Sheria ya ushuru wa thamani VAT, Sheria ya Fedha na viwango vipya vya ushuru wa bidhaa.

    Mamlaka hiyo imeongeza kuwa serikali itatumia takriban Shilingi bilioni 5 za Kenya kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Petroli kusaidia kupunguza makali ya ongezeko la bei ya dizeli na mafuta ya taa kwa watumiaji.

    Katika kipindi kilichopita, petroli ilikuwa ikiuzwa kwa Shilingi 197.60 kwa lita pesa za Kenya huku dizeli ikiuzwa kwa Shilingi 196.63 za Kenya baada ya kupunguzwa kwa Shilingi 9.37 na Shilingi 10.21 mtawalia za Kenya.

    Tangazo hili jipya linajiri wakati soko la mafuta duniani likiendelea kubadilika na huku gharama ya maisha ikiendelea kuongezeka.

    Soma zaidi:

  8. Trump asema China sasa kununua mafuta Marekani na kutoipatia silaha Iran

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema mazungumzo ya biashara kati ya Marekani na China “yamekwenda vizuri zaidi kuliko mara ya mwisho”, akieleza kuwa safari hii yalikuwa makubwa zaidi kuliko makubaliano 36 yaliyosainiwa katika mazungumzo yaliyopita.

    Trump amesema China itanunua kiasi kikubwa cha mazao ya kilimo kutoka Marekani, ikiwemo maharage ya soya.

    Alipoulizwa na mtangazaji wa Fox News Sean Hannity kuhusu kile ambacho China inataka kutoka Marekani, Trump alijibu: “Ni mambo mengi sana ya kujadili, lakini yapo mengi,” bila kutoa maelezo zaidi.

    Katika mazungumzo hayo, Trump pia amesema China imekubali kununua mafuta kutoka Marekani.

    “Tutaona meli za China zikielekea Texas, Louisiana na Alaska,” anasema, akiongeza kuwa nishati ndiyo bidhaa ambayo China inaihitaji zaidi.

    “Tunayo nishati isiyo na kikomo,” alisema.

    Sasa zaidi kuhusu vita vya Iran, Trump anasema aliwaambia wenzake wa China kwamba Marekani ilikuwa "ikiwasaidia" kweli.

    "Sidhani kama China inataka Iran iwe na silaha ya nyuklia," Trump anasema.

    Trump pia amedai kuwa Rais wa China Xi Jinping amekubali kununua ndege 200 za kampuni ya Boeing, akieleza hatua hiyo kama “ahadi kubwa”.

    “Ndege 200 kubwa, hiyo ni ajira nyingi. Boeing walitaka 150, lakini wamepata 200,” alisema.

    Mapema, Waziri wa Hazina wa Marekani alikuwa amedokeza uwezekano wa China kutangaza oda kubwa ya ndege za Boeing, akiiambia CNBC kuwa Beijing huenda ikatangaza rasmi ununuzi huo hivi karibuni.

    Trump amehitimisha kwa kusema amefanikisha zaidi kuliko viongozi wengine katika kushughulikia biashara na China, akidai nakisi ya biashara kati ya nchi hizo imepungua kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na ilivyokuwa awali.

    Trump na wafanyibiashara alioandamana nao China watakamilisha ziara yao hii leo.

    Soma zaidi:

  9. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya Ijumaa ya tarehe 15 Mei 2026.