Mkuu wa WHO atembelea Uganda huku mlipuko wa Ebola ukienea kutoka DR Congo

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus amewasili Uganda huku mamlaka ikiongeza juhudi za kudhibiti mlipuko wa Ebola unaohusishwa na nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Uganda imethibitisha visa vinavyohusishwa na maambukizi ya kuvuka mpaka, huku maafisa wa afya wakiimarisha ufuatiliaji kwenye mpaka wake wa magharibi.
Aliongeza kuwa mifumo ya afya ya Uganda inafanya kazi kwa ufanisi katika maeneo muhimu ya kudhibiti milipuko.
Wakati wa ziara yake, Dkt Tedros alisifu mwitikio wa nchi, akisema Uganda imechukua "hatua za haraka na zenye uwezo mkubwa" kwa mlipuko huo, akiangazia jukumu la uchunguzi wa mpaka katika kubaini maambukizi kutoka nchi ya DRC.
Kati ya maambukizi19 yaliothibitishwa nchini Uganda hadi sasa, 14 yanahusisha watu walioingia kutoka DRC, wakati watano ni raia wa Uganda. Vifo viwili vimerekodiwa kati ya wale waliovuka mpaka.
"Tuko pamoja na familia zao kipindi hiki kigumu," Dk Tedros alisema, akiongeza kuwa WHO inaunga mkono Uganda pamoja na Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) na washirika wengine wa kikanda.
"Kwa ushirikiano unaoendelea, nina imani janga hili linaweza kudhibitiwa," alisema.
Hali nchini Uganda inafungamana kwa karibu na mlipuko unaoendelea mashariki mwa DRC, ambao kufikia sasa umeingia wiki yake ya nne.
Mamlaka za afya huko zilisema watu 12 wamepona ugonjwa wa Ebola wa Bundibugyo, wakati wagonjwa 283 bado, ama wametengwa au wanapokea matibabu katika maeneo 25 ya afya katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Upimaji wa maabara umethibitisha sampuli chanya 515 tangu mlipuko huo ulipotangazwa, na vifo 91 vimerekodiwa.
Jitihada za kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo zimekumbwa na changamoto za ukosefu wa usalama na upatikanaji wa vifaa katika maeneo ya mashariki mwa Congo, ambapo makundi yenye silaha yanaendeleza shughuli zake na kufikia baadhi ya maeneo ya vituo vya afya ni changamoto.
Soma zaidi:























