Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) kutoka Tabora hadi Kigoma yenye urefu wa kilomita 506, mradi ambao serikali inasema utakuwa kiungo muhimu katika kuimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.
Kipande hicho cha reli, chenye thamani ya takribani shilingi trilioni 6.23 (sawa na dola za Marekani bilioni 2.4), kitaiunganisha Kigoma na mtandao wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam, hatua inayolenga kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kupitia Bandari ya Dar es Salaam kwenda Burundi na mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kwa mujibu wa serikali, reli hiyo itakapokamilika, safari ya abiria kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma itachukua takribani saa saba hadi nane, ikilinganishwa na takribani saa 40 zinazotumika sasa kupitia reli ya kati ya kawaida.
Serikali pia inasema usafirishaji wa mizigo kwenda mashariki mwa DRC utakuwa wa haraka zaidi kuliko usafiri wa malori, ambao kwa sasa unaweza kuchukua kati ya siku nne na saba kutegemeana na eneo la mwisho la mzigo na hali ya barabara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Samia alisema uwekezaji katika miundombinu ya uchukuzi unalenga kuiunganisha Tanzania na masoko ya kikanda.
"Kijiografia, nchi yetu ni lango la biashara kwa nchi jirani zinazotuzunguka. Kwa msingi huo, kila tunapojenga reli, viwanja vya ndege, bandari au barabara, hatuunganishi mikoa yetu pekee, bali tunaiunganisha pia nchi yetu na fursa za masoko ya Afrika Mashariki, Afrika ya Kati na Kusini mwa Afrika."
Serikali inasema mradi huo unatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 15,000 wakati wa ujenzi na kuchochea uwekezaji, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi katika mikoa ya Tabora na Kigoma.
Changamoto za utekelezaji
Pamoja na matarajio hayo, upanuzi wa mtandao wa SGR nchini umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo upatikanaji wa fedha. Baadhi ya vipande vya reli vimeendelea kwa kasi, huku vingine vikichelewa kutokana na changamoto za ufadhili na utekelezaji.
Kwa mujibu wa serikali, ujenzi wa kipande cha Tabora–Kigoma umefikia zaidi ya asilimia 10 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 48, sawa na miaka minne, ifikapo mwaka 2030.
Hata hivyo, wadau wa sekta ya uchukuzi wataendelea kufuatilia iwapo ratiba hiyo itaweza kutekelezwa, ikizingatiwa changamoto zilizojitokeza katika baadhi ya miradi mingine ya SGR, zikiwemo gharama za ujenzi, upatikanaji wa fedha na uratibu wa miundombinu mingine kama bandari na usafiri wa majini.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa kujenga mfumo jumuishi wa uchukuzi.
"Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika reli ya kisasa ya SGR, bandari, viwanja vya ndege na usafiri wa majini kwa lengo la kujenga mfumo jumuishi wa uchukuzi unaounganisha maeneo ya uzalishaji, masoko ya ndani na nchi jirani.
Uwekezaji huu unaendelea kuiweka Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji, biashara na huduma za ugavi katika Afrika Mashariki na Kati."
Ushindani wa njia za biashara
Mradi huo unatekelezwa wakati ushindani wa njia za biashara katika Afrika Mashariki na Kati ukiendelea kuongezeka.
Tanzania inalenga kuimarisha nafasi ya Central Corridor, inayotumia Bandari ya Dar es Salaam, huku ikishindana na Northern Corridor inayopitia Bandari ya Mombasa nchini Kenya, pamoja na Lobito Corridor inayounganisha Angola, Zambia na DRC kwa lengo la kuvutia biashara ya madini.
Iwapo reli ya Tabora–Kigoma itakamilika kwa wakati na kuunganishwa kikamilifu na bandari pamoja na usafiri wa majini katika Ziwa Tanganyika, inaweza kuimarisha nafasi ya Tanzania kama lango muhimu la biashara kwa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.