Shughuli za
usafiri zimeendelea kutatizika katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jommo
Kenyatta nchini Kenya kwa siku ya pili Jumatatu hii, maelfu ya wasafiri
wakilalamikia kuahirishwa kwa safari zao au nyingine kukwama wasijuwe
watasafiri lini.
Uwanja huu
ndio wenye shughuli nyingi kabisa katika ukanda wa Afrika Mashariki na maziwa
makuu, ukiwa na wasafiri 13,000 kila siku, huku watu milioni 8.6 wakisafiri
kupitia uwanja huo kila mwaka huku ndege 200 zikitua uwanjani humo na nyingine
195 zikiondoka.
Baadhi ya
wasafiri wameelezea mahangaiko ya kusubiri hadi saa 10 katika uwanja wa ndege
ili kusafiri.
Hapo jana
mamlaka ya kusimamia viwanja vye ndege KAA ilitoa taarifa kusema kuwa
inashughulikia suala hilo kupunguza mahangaiko ya wasafiri katika viwanja vya
ndege lakini hali hiyo imeendelea kukumba viwanja vyote vya ndege vya umma
nchini Kenya kutokana na mgomo wa wafanyakazi wa viwanja vye ndege.
Akizungumza
na BBC mapema Jumatatu, Bwana Moss Ndiema amesema kwamba wana mengi ya
kulalamikia ila masuala makuu matatu yamewalzaimu kurejelea mgomo miezi michache
tu baada ya KAWU kuafikiana na serikali ya Kenya kusitisha mgomo mwingine.
Kulingana na
KAWU, Mamlaka ya kudhibiti mishahara ya watumishi wa umma nchini Kenya SRC
iliiamrisha Mamlaka ya Usafiri wa Anga Kenya KCAA kutumia moja kati ya mikataba
mitatu ya makubaliano yaliyotiwa Saini kati ya 2015 na 2025.
Mpango huu
ungeangazia suala la nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi wa viwanja wa ndege
ambao wamelalamikia kutopata nyongeza hiyo tangu 2015.
Hatua ya
Mkurugenzi wa Mamlaka ya kusimamia viwanja vya ndege KAA Moses Wekesa kuwatumia
maafisa wa huduma ya vijana NYS kutekeleza majukumu ya Ulinzi wa viwanja ambao
KAWU imesema ni jukumu la maafisa wa KAA limewakera mno wakimtaka kuondolewa
kazini kwa ajili ya kile wamekitaja kama kiburi na dharau kwao.
Suala la
tatu ambalo wamesema ni muhimu kwao ni wafanyakazi wa kampuni ya ndege ya Jambo Jet ambayo inamilikiwa na shirika la ndege nchini Kenya – Kenya Airways. Jambo
Jet imedaiwa kutowaruhusu wafanyakazi wake kujiunga na vyama vya wafanyakazi
kama vile KAWU , hali ambayo wamedai inawanyimanafasi ya kutetea haki zao
ambazo KAWU inasema inadhulumiwa kazini.
Na japo
Katibu Mkuu Ndiema amesema wasafiri wanaendelea kuhangaika uwanjani kwa kuwa
safari zao zimeahirishwa au kukwama, inawabidi kufanya hivyo kwa ajili ya
kupata haki yao ya kikatiba.
‘Ni
masikitiko makubwa lakini hatuna budi ila kuilazimu serikali kuketi nasi chini
mezani na kutatua mzozo huu ambao sasa tunahisi umekuwa mbaya zaidi kwetu,’
alisema Bwana Ndiema kwenye mahojiano ya simu n BBC.
Katika
uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta,
wasafiri waliendelea kulalmikia kukwama kwa siku ya pili Jumatatu.
Siku ya
Jumapili wengi waliwaeleza wanahabari kuhusu hali ya kukata tamaa. Kulingana na badhi ya wasafiri, hali hiyo
iliwapata kwa mshtuko mkubwa.
Nicole
Jepkorir, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 24 anayesoma katika chuo kikuu nje ya
Kenya amesema; "Tulitakiwa kuondoka
saa kumi jioni leo, lakini kutokana na usumbufu na maandamano yaliyokuwepo hapa
asubuhi ya leo, tutaondoka saa sita usiku. Hali hii inaleta usumbufu mkubwa kwa
sababu tulifika hapa mapema sana asubuhi.
Tulitakiwa kuwa tumekamilisha
taratibu za kuingia kwenye ndege (check-in) kufikia sasa, lakini hatuwezi
kufanya hivyo. Hatuna la kufanya kwa sababu KAA [Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Kenya] inapaswa kupokea ndege ili ziweze kuja kutuchukua na kuondoka; kwa hivyo
hakuna kinachoendelea. Tunapata taarifa kwa kuchelewa; kama tungeambiwa mapema,
tusingekuja hapa. Labda tungekuja wakati ambao tulitakiwa kuondoka."
Naye William
Obino, ambaye ni mwanafunzi pia amesema,"Tulitakiwa kukamilisha taratibu za kuingia kwenye ndege (check-in)
majira ya saa sita mchana na kuondoka saa kumi jioni, lakini safari yetu ya
ndege sasa imecheleweshwa hadi saa sita usiku. Kuna watu wengi waliokwama hapa,
ikiwemo sisi wenyewe, kwa hivyo ni jambo la kusikitisha sana."
William
Obino, mwenye umri wa miaka 22 amesema kwamba ;"Imetuathiri sana kwa sababu inavuruga ratiba yetu; tulikuwa na
ratiba iliyopangwa kwa ajili ya siku zote za safari yetu, na sasa kutokana na
kuchelewa huku, huenda tukalazimika kuondoa baadhi ya mambo kwenye ratiba
hiyo."
Hazikizimana
Lolewi Spoil, mfanyabiashara kutoka Rwanda amesema ; "Nilipaswa kusafiri
saa 11 jioni, lakini nilipofika hapa, nilipokea barua pepe ikisema kuwa kuna
ucheleweshaji na kwamba safari yangu ya ndege imeahirishwa hadi saa 5 usiku.
Nilipomuuliza mmoja wa wafanyakazi, aliniambia ni kweli, na kwamba tunapaswa
kuwa na subira na kusubiri hadi wakati huo."
KAWU imesema
inatarajiwa kukutana na Waziri wa uchukuzi wa umma nchini Kenya davis Chirchir,
Katibu wake Teresiah Mbaika, Maafisa kutoka wizara ya Leba, Maafisa wa Mamlaka
za KCAA na KAA na Katibu Mkuu wa vyama vya wafanyakazi nchini kenye, COTU
Francis Atwoli kujaribu kutatua mzozo uliopo..