Tanzania yaongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia mara 3
- Author, Yusuph Mazimu
- Nafasi, BBC Swahili
Upatikanaji wa nishati safi ya kupikia nchini Tanzania umeongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 23.2 mwaka 2025, hilo ni ongezeko la zaidi ya mara tatu ndani ya kipindi cha miaka minne.
Taarifa hiyo ilitolewa wiki hii na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, wakati wa Mdahalo wa Ngazi ya Juu wa Mawaziri ulioandaliwa na Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA) jijini Paris, Ufaransa.
Ndejembi alisema mafanikio hayo yanaakisi dhamira ya serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi, salama na nafuu kwa ajili ya kupikia, huku yakichangia kulinda afya za wananchi, mazingira na kukuza uchumi wa taifa.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, mafanikio hayo yamechangiwa na utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Kwanza wa Afrika wa Nishati Safi ya Kupikia, ambapo Tanzania ilishiriki kuhamasisha ahadi ya dola za Marekani bilioni 2.2 kwa ajili ya kuendeleza sekta hiyo barani Afrika.
Aidha, alisema uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034 umeweka msingi wa kuimarisha sera, kanuni, mifumo ya kifedha na ushiriki wa sekta binafsi katika kuongeza matumizi ya nishati safi nchini.
“Kwa mwaka huu wa fedha, Serikali inatarajia kusambaza majiko banifu 200,000 na mitungi 450,000 ya gesi ya LPG kwa ruzuku, pamoja na kuanza majaribio ya mfumo wa kulipia vifaa vya kupikia kwa umeme kupitia bili za Shirika la Umeme Tanzania, ili kupunguza gharama za awali kwa wananchi,” amesema Ndejembi.
Wakati serikali ikiendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi, baadhi ya wananchi wanaamini mpango huo unaweza kuwa na mchango mkubwa katika juhudi za kuhifadhi mazingira.
Aboubakar Shemdoe, mkazi wa Tanga, amesema matumizi ya nishati safi yanaweza kuwa miongoni mwa hatua muhimu zaidi katika kupunguza uharibifu wa mazingira nchini.
“Kama kuna kitu serikali itafanikiwa kwenye kutuza mazingira basi ni matumizi ya nishati safi,” amesema.
Kwa upande wake, mdau wa nishati jadidifu, Shima Sago, amesema matumizi makubwa ya mkaa yanaendelea kuwa changamoto kubwa kwa mazingira nchini.
“Matumizi ya mkaa Tanzania yamekuwa makubwa sana sasa hivi tunatumia tani milioni 2.5 kwa mwaka,” amesema.
Sago amesema kiwango hicho cha matumizi kina athari kubwa kwa misitu kutokana na idadi ya miti inayohitajika kuzalisha mkaa.
“Tani 12 za miti inakupa tani 1 ya mkaa, kwa tani 2.5 milioni za mkaa, utaona ni kiasi gani cha miti inakatwa kila mwaka,” amesema.
Wataalamu wanaeleza kuwa kupungua kwa utegemezi wa mkaa na kuni kunaweza kusaidia kupunguza kasi ya ukataji miti, kuhifadhi bioanuwai na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mbali na athari za mazingira, matumizi ya nishati za jadi yanaendelea kuwa changamoto ya afya ya umma duniani. Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa watu milioni 2.9 hufariki dunia kila mwaka kutokana na magonjwa yanayohusishwa na uchafuzi wa hewa majumbani unaosababishwa na matumizi ya nishati zisizo safi kama kuni na mkaa.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazotekeleza mikakati ya kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kuboresha afya za wananchi, kupunguza uharibifu wa mazingira na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.