Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Marekani yawataka raia wake nchini Bahrain kuwa 'waangalifu'

Ubalozi wa Marekani nchini Bahrain watahadharisha kuwa Iran imekuwa ikishambulia nchi hiyo na kuwataka raia wake kujihifadhi

Moja kwa moja

Sarafina Robi & Mariam Mjahid

  1. Na kufikia hapo tunatamatisha matangazo yetu ya moja kwa moja. Alamsiki.

  2. Marekani yawataka raia wake nchini Bahrain kuwa 'waangalifu'

    Ubalozi wa Marekani nchini Bahrain ulitoa tahadhari ya kiusalama, ukiwataka raia wa Marekani walioko nchini humo na katika eneo hilo "kuwa waangalifu zaidi."

    Katika ujumbe uliowekwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, ubalozi huo wa Marekani ulikumbusha: "Hapo awali Iran imewahi kulenga miundombinu ya kiraia nchini Bahrain, ikiwemo hoteli jijini Manama."

    Ubalozi huo ulisema raia wa Marekani katika eneo hilo wanapaswa kujiandaa kwa "uwezekano wa kughairiwa kwa safari za ndege, kufungwa kwa anga, na kukwama kwa safari."

    Wakati huo huo, shirika la habari la serikali ya Bahrain liliripoti kuwa Waziri wa Mambo ya Nje Abdullatif bin Rashid Al-Zayani alifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdel Ati, kuhusu uhusiano wa nchi hizo mbili na hali katika Mlango-bahari wa Hormuz.

    Kwa mujibu wa ripoti hiyo, pande hizo mbili zilijadili athari za kukwama kwa usafirishaji wa meli kwenye biashara ya kimataifa na kusisitiza "umuhimu wa kuimarisha juhudi za kikanda ili kusaidia usalama na utulivu katika eneo hilo."

  3. Niger yaishutumu Ufaransa kwa kupanga mapinduzi nchini humo

    Mamlaka za Niger zimelituhumu rasmi taifa la Ufaransa kwa kuunga mkono kile zilichokitaja kuwa "jaribio la kuvuruga utulivu wa nchi hiyo mnamo tarehe 28 na 29 Agosti."

    Katika taarifa yake, serikali ya Niger ilisema kuwa makabiliano yaliyotokea katika Kituo cha Jeshi la Anga cha 101 jijini Niamey yalikuwa na "athari za kimataifa," na kuongeza kuwa "mashahidi wengi wamehojiwa kuhusiana na shambulio hilo, na serikali inafikiria kuwasilisha malalamiko katika mahakama za kimataifa."

    Taarifa hiyo pia ilisema kuwa "Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anaongoza muungano mpana wa watu binafsi na mashirika yanayounga mkono operesheni hii," huku ikidai kuwa baadhi ya nchi za Afrika ambazo hazikutajwa majina zilichukua nafasi ya upatanishi.

    Hata hivyo, hadi sasa, serikali ya Niger haijawasilisha ushahidi wowote kuthibitisha madai hayo. Kituo cha Jeshi la Anga cha 101, ambacho kilishambuliwa tarehe 29 Agosti, ni sehemu ya eneo la uwanja wa ndege wa Diori Hamani.

    Kituo hicho kinahifadhi ndege za kijeshi na ndege zisizo na rubani (drones) za Niger, pamoja na kikosi cha kupambana na ugaidi kutoka muungano wa nchi za Sahel.

    Shirika la habari la Reuters liliripoti kuwa wanajeshi wa Urusi na Italia pia wana vituo vyao katika eneo hilo.

    Niger ilisema kuwa mbali na Urusi, pia ilipokea msaada kutoka Algeria. Urusi imethibitisha kuwa vikosi vyake vilisaidia kuzima kile kilichoelezewa kuwa jaribio la mapinduzi nchini Niger siku ya Jumamosi.

  4. Zaidi ya watu 60 wauawa katika mapigano Yemen

    Zaidi ya watu 60 wameuawa katika mapigano kati ya vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia na waasi wa Houthi nchini Yemen, kwa mujibu wa vyanzo vya kitabibu na kijeshi vilivyonukuliwa na AFP.

    Vyanzo hivyo vimesema raia pia ni miongoni mwa waliouawa.

    Kwa mujibu wa AFP, wanajeshi 26 wa serikali waliuawa katika mapigano yaliyodumu kwa saa kadhaa kusini magharibi mwa Yemen, huku Wahouthi wakiripoti vifo vya wapiganaji wao 31.

    Katika mji wa Taiz unaodhibitiwa na serikali, watu sita waliuawa na wengine saba kujeruhiwa baada ya kombora kushambulia basi.

    Wahouthi, wanaojiita Ansar Allah, wanadhibiti maeneo makubwa ya kaskazini mwa Yemen na pwani ya magharibi kwenye Bahari Shamu, pamoja na mji mkuu Sanaa.

    Serikali inayotambuliwa kimataifa inaongozwa na Baraza la Uongozi la Rais na linaungwa mkono na Saudi Arabia. Linadhibiti maeneo ya mashariki mwa Yemen na pwani ya kusini, ikiwemo bandari ya Aden.

  5. Moto uliozuka Mlima Kilimanjaro wadhibitiwa kwa asilimia 90

    Moto umezuka katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro nchini Tanzania,huku waziri wa Maliasili na Utalii nchini humo Dkt. Ashatu Kijaji,akisema kuwa moto huo umedhibitiwa kwa asilimia 90.

    Kijaji alitembelea eneo hilo lililoathirika siku ya Jumamosi ili kutathmini hali na jitihada za kuuzima moto huo.

    Alisema chanzo cha moto huo bado hakijajulikana na kwamba uchunguzi unaendelea, "Jitihada za kuuzima moto huo kabisa zinaendelea na tunatarajia kuwa sehemu iliyobaki itazimwa kabla ya mwisho wa leo (Jumamosi)," alisema.

    Kijaji pia aliwataka wakazi wanaoishi karibu na eneo hilo la hifadhi kuepuka shughuli zinazoweza kusababisha moto na kuharibu mazingira pamoja na wanyamapori.

    Moto huo ulianza kuwaka majira ya saa tisa na nusu alasiri (15:30) kwa saa Afrika Mashariki (saa 12:30 GMT) siku ya Alhamisi katika eneo la Kikerelwa, upande wa kaskazini mashariki mwa mlima huo katika Wilaya ya Rombo.

    Hii si mara ya kwanza kwa Mlima Kilimanjaro kukumbwa na tatizo la moto. Mnamo mwezi Septemba 2023, moto uliowaka kwa takriban wiki moja uliharibu eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 17, sawa na takriban asilimia 1 ya eneo la hifadhi ya mlima huo.

    Moto mwingine mwaka 2022 uliendelea kwa takriban mwezi mmoja na kuharibu maelfu ya hekta za msitu inayozunguka mlima huo. Mlima Kilimanjaro una urefu wa karibu mita 5,900 kutoka usawa wa bahari na ni mojawapo ya vivutio maarufu zaidi vya utalii nchini Tanzania.

  6. Muhoozi ataka wanaoenda haja ndogo hadharani wachukuliwe sheria

    Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ametoa onyo kali dhidi ya wanaume wanaojisaidia kando ya barabara, akitaka wakamatwe mara moja na kufungwa kwa angalau miaka mitano.

    Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, Jenerali Muhoozi, ambaye ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni, amesema wanaume wanaokojoa kando ya barabara mbele ya watu, wakiwemo watoto, wanapaswa kukamatwa mara moja.

    “Wanaume wote wanaojisaidia kando ya barabara mbele ya watu, wakiwemo watoto, lazima wakamatwe mara moja. Watafungwa kifungo kisichopungua miaka mitano,” Kainerugaba alisema.

    Kauli hiyo imezua mjadala mkubwa mtandaoni, huku baadhi ya watu wakiunga mkono hatua kali za kukabiliana na uchafuzi wa mazingira na wengine wakihoji ukali wa adhabu hiyo.

    Wanaounga mkono msimamo huo wanasema kukojoa hadharani kunahatarisha usafi wa mazingira, kuwa mfano mbaya kwa watoto na kuharibu maeneo ya umma.

  7. Iran yawataka Wamarekani kupinga vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Ismail Baghaei, amewataka raia wa Marekani kutoruhusu serikali yao “kuwafanya wanajeshi wa mstari wa mbele katika vita.”

    Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, Baghaei aliwataka Wamarekani kutokubali kutumwa vitani katika vita wanavyolipia na ambavyo hawakuchagua, akisema pia wasiruhusu watoto wao kufanywa mamluki katika kile alichokiita vita haramu.

    Hapo awali, Rais Donald Trump aliwaambia waandishi wa habari Ijumaa kuwa Marekani iko karibu sana kuushambulia Mlima Kalang nchini Iran.

    Mlima Kalang, uliopo karibu na kituo cha kurutubisha uranium cha Natanz, ni eneo lenye ulinzi mkali na miundombinu miwili ya chini ya ardhi yenye kina kirefu.

    Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Trump alisema vita na Iran “si jambo kubwa sana” kwa Marekani, akisema anapendelea kukiita “makabiliano ya kijeshi”.

  8. Marekani kuuza silaha zenye thamani ya dola bilioni 5 kwa Saudi Arabia

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetangaza kuidhinisha makubaliano ya kuiuzia Saudi Arabia silaha zenye thamani ya dola bilioni 5.

    Katika taarifa, wizara hiyo imesema imeidhinisha ombi la Saudi Arabia la kununua maelfu ya mabomu pamoja na mifumo ya kuongoza makombora ya masafa marefu.

    Kwa mujibu wa wizara hiyo, makubaliano hayo pia yanajumuisha silaha mbalimbali, vipuri na kemikali, pamoja na huduma za kiufundi na kimkakati za usafirishaji na ugavi.

    Marekani imesema makubaliano hayo yanalenga kuimarisha usalama wa mshirika wake muhimu, huku yakisaidia kudumisha utulivu wa kisiasa na maendeleo ya kiuchumi katika eneo la Ghuba.

    Wizara hiyo imeongeza kuwa makubaliano hayo yataimarisha uwezo wa Saudi Arabia wa kujilinda dhidi ya mashambulizi ya anga na kukabiliana na vitisho vinavyoikabili eneo hilo.

    Soma Zaidi:

  9. Wajumbe wa amani wa Trump kuzuru Moscow na Kyiv

    Wapatanishi wa Marekani, Steve Witkoff na Jared Kushner, watazuru Urusi na Ukraine wikendi hii, huku juhudi za kuhitimisha vita zikionekana kushika kasi.

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, alithibitisha kuwa atakutana na wajumbe hao siku ya Jumapili, baada ya wao kutembelea Moscow siku ya Jumamosi kwa ajili ya mazungumzo na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.

    Witkoff na Kushner wameongoza juhudi za Rais wa Marekani Donald Trump za kufanikisha makubaliano ya amani, lakini bado kuna pengo kubwa kati ya pande hizo mbili zinazopigana. "Wanakuja na pendekezo la kuhitimisha vita," Trump aliwaambia waandishi wa habari alipoulizwa kuhusu ziara hizo.

    Mapema siku ya Ijumaa, Zelensky alisema ndege isiyo na rubani ya Urusi ilishambulia ofisi ya mkuu wa usalama wa Ukraine, Oleksandr Poklad, mjini Kyiv. Poklad anaonekana kuwa salama na hajajeruhiwa.

    Katika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, Zelensky alisema amemwagiza Poklad, ambaye anaongoza idara ya usalama ya SBU, kuchukua hatua stahiki kujibu shambulio hilo.

    Siku ya Jumamosi, mamlaka za eneo hilo zilisema watu wanne waliuawa katika shambulio la Urusi dhidi ya mji wa Kamianske, ulioko kusini-mashariki mwa nchi hiyo. Witkoff na Kushner, ambaye ni mkwe wa Trump, wamekuwa Urusi mara kadhaa, lakini mazungumzo hayo yanayotarajiwa yatakuwa ya kwanza kufanyika nchini Ukraine.

    Zelensky alisema atahakikisha usalama wa anga la Urusi wakati wa ziara ya wajumbe hao na kuitaka Urusi kufanya vivyo hivyo kwa upande wa Ukraine. Wakati huo huo, Putin aliambia kongamano la kimataifa la uchumi siku ya Alhamisi kuwa "kuna uwezekano" wa kufikiwa kwa makubaliano ya amani.

  10. Trump: Huenda tukashambulia Mlima Kalang hivi karibuni

    Siku ya Ijumaa, Donald Trump aliwaambia waandishi wa habari kuwa Marekani inaweza kuushambulia Mlima Kalang nchini Iran hivi karibuni.

    Mlima Kalang, uliopo karibu na kituo cha kurutubisha urani cha Natanz, ni eneo lililolindwa sana la kijeshi lenye mifumo miwili ya mahandaki ya kina kirefu.

    Katika sehemu nyingine ya maelezo yake, Rais huyo wa Marekani alisema kuwa vita dhidi ya Iran ni "jambo dogo" kwa Marekani.

    Awali, Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance alisema siku ya Alhamisi kuwa asingeliita mgogoro na Iran kuwa ni "vita."

    Siku ya Ijumaa, Donald Trump alitoa ufafanuzi alipoulizwa na mwandishi wa habari awaeleze wananchi wa Marekani maana ya vita na Iran ikiwa hali hiyo haitaitwa "vita", alisema, "Naam, nawaambia, watu wengi hawaiiti hali hi kuwa vita.

    Mimi naiita mgogoro wa kijeshi, kwa sababu kwetu sisi ni jambo dogo kiasi. Sio jambo kubwa. Tulichukua hatua nchini Venezuela na tukafanikiwa. Hatukupoteza maisha ya watu nchini Venezuela.

    Tulipoteza watu 18 katika mgogoro na Iran. Tulipoteza watu 100,000 nchini Vietnam."

  11. Umoja wa Mataifa wapitisha ramani mpya ya Afrika

    Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepiga kura ya kuidhinisha kubadilishwa kwa ramani ya kawaida ya dunia na kuweka nyingine inayoonyesha ukubwa halisi wa bara Afrika.

    Azimio hilo lenye lengo la "Kurekebisha Ramani," lililowasilishwa na Togo na kuungwa mkono na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), lilipitishwa kwa uungwaji mkono wa mataifa 164, yakiwemo Ufaransa na Uingereza.

    Marekani ndiyo nchi pekee iliyopiga kura ya kupinga, huku nchi sita zikijizuia kupiga kura. Ingawa kura hiyo ya Umoja wa Mataifa haina nguvu ya kisheria ya kulazimisha utekelezaji, itasababisha mabadiliko katika ramani zinazotumiwa na taasisi mbalimbali duniani kote.

    Ramani ya Mercator, ambayo imekuwa ikitumika sana tangu karne ya 16, imekabiliwa na ukosoaji kwa sababu inaonyesha Afrika kuwa na ukubwa sawa na Greenland, licha ya ukweli kwamba Afrika ni kubwa mara 14 zaidi ya Greenland.

    Wakosoaji wanasema hali hii inasababisha kupuuzwa kwa mahitaji ya maendeleo na uwezo wa nchi zilizo karibu na ikweta.

    Ramani ya Mercator iliundwa mwaka wa 1569 na mtengenezaji wa ramani kutoka Flanders, Gerardus Mercator, ili kuwasaidia wavumbuzi wa Ulaya kusafiri kote duniani.

    Upotoshaji katika ramani yake unatokana na ukweli kwamba haiwezekani kuwakilisha kwa usahihi uso wa dunia kwenye ramani ya pande mbili.

  12. Hujambo, natumai umzima, karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya 05/09/2026.