Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Trump apiga marufuku CNN na Politico White House

Rais wa Marekani Donald Trump alidai kuwa vyombo hivyo mara kwa mara huchapisha au kuripoti taarifa za uongo kuhusu utawala wake bila kuthibitisha madai hayo.

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi

  1. Moshi mnene waripotiwa kufuka karibu na uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Riyadh

    Moshi mweusi umeonekana ukifuka karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Riyadh saa chache baada ya tahadhari za mashambulizi ya anga kutolewa katika mji mkuu wa Saudi Arabia.

    Hii ni mara ya kwanza kwa wakazi wa Riyadh kupewa tahadhari rasmi na kuagizwa kusalia majumbani mwao tangu kuongezeka kwa mvutano wa hivi karibuni kati ya Saudi Arabia na waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran nchini Yemen.

    Baadaye, milipuko kadhaa ilisikika katika maeneo mbalimbali ya mji huo, huku matatizo makubwa yakiripotiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Khalid.

    Shirika la habari la Reuters, likimnukuu mashuhuda wa tukio hilo, lilisema moshi huo ulionekana katika eneo jirani na uwanja huo wa ndege katika mji mkuu wa Saudi Arabia.

    Hata hivyo, serikali ya Saudi Arabia haijatoa tamko rasmi kuhusu tukio hilo wakati Reuters ilipowasilisha ripoti yake.

    Mwandishi wa AFP alishuhudia wazima moto wakipambana kuzima moto katika tanki la mafuta lililoteketea karibu na Riyadh. Tangi hilo linamilikiwa na Aramco, kampuni ya mafuta na gesi inayomilikiwa na serikali ya Saudi Arabia.

    Usiku wa kuamkia Jumamosi, Idara ya Ulinzi wa Kiraia ya Saudi Arabia ilituma tahadhari kupitia simu za mkononi, ikiwataka wakazi wa Riyadh na maeneo mengine kuwa waangalifu. Hata hivyo, asubuhi ilitangaza kuwa hali ilikuwa salama.

    Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa tahadhari ya aina hiyo kutolewa katika mji mkuu wa Saudi Arabia tangu kuongezeka kwa mvutano kati ya Saudi Arabia na Wahouthi wa Yemen.

    Siku ya Ijumaa, waasi wa Houthi walidai kuwa walizuia mashambulizi ya Saudi Arabia dhidi ya mji mkuu wa Yemen, Sanaa. Kundi hilo lilisema mashambulizi hayo yalifanana kwa mbinu na operesheni zinazotekelezwa na kundi la Islamic State (IS).

    Unaweza kusoma:

  2. Iran yatekeleza hukumu ya kifo dhidi ya mtuhumiwa wa ujasusi wa Isarel

    Mhimili wa mahakama nchini Iran umetangaza kutekelezwa kwa hukumu ya kifo dhidi ya Hossein Pedaran, raia wa Iran aliyepatikana na hatia ya kuifanyia Israel ujasusi.

    Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mizan, linalohusishwa na idara ya mahakama, Pedaran alishtakiwa kwa kuipatia Mossad, shirika la ujasusi la Israel, taarifa kuhusu maeneo nyeti ya kijeshi katika mkoa wa Isfahan.

    Mizan ilisema ushahidi uliowasilishwa dhidi yake ulijumuisha vifaa vilivyokamatwa pamoja naye na maelezo ya kukiri makosa. Mashtaka dhidi yake yalihusisha ujasusi na ushirikiano wa kiintelijensia kwa manufaa ya Israel, pamoja na madai ya kuanzisha mawasiliano na kuonyesha nia ya kushirikiana na mashirika ya ujasusi ya Marekani.

    Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hukumu ya kifo ilitekelezwa baada ya kuidhinishwa na Mahakama ya Juu ya Iran.

    Hata hivyo, taarifa ya mahakama haikubainisha tarehe ya kukamatwa kwa Pedaran, mahali kesi yake iliposikilizwa wala maelezo ya ushahidi yaliyowasilishwa mahakamani.

    Pia soma:

  3. Trump asaini sheria ya vikwazo dhidi ya Urusi na Iran

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesaini sheria mpya inayoweka vikwazo vikali zaidi dhidi ya Urusi na kuimarisha vikwazo vilivyopo dhidi ya Iran.

    Sheria hiyo inaongeza shinikizo dhidi ya Moscow kwa kupanua wigo wa vikwazo, ushuru na hatua nyingine za kiuchumi, huku pia ikiendeleza vikwazo vya Marekani dhidi ya Tehran.

    Mapema wiki hii, Bunge la Wawakilishi la Marekani lilipitisha mswada huo kabla ya kuuwasilishwa kwa rais kutiwa saini.

    Sheria hiyo inalenga maafisa wa Urusi, taasisi za kifedha na mashirika mengine ya nchi hiyo. Pia inahusisha hatua zinazogusa sekta za nishati na biashara za Urusi, huku ikimpa rais wa Marekani mamlaka ya kutoza ushuru wa hadi asilimia 100 kwa nchi zinazoagiza kwa kiwango kikubwa mafuta na gesi asilia kutoka Urusi.

    Sheria hiyo pia inaongeza muda wa utekelezaji wa Sheria ya Vikwazo dhidi ya Iran ya mwaka 1996 kwa kipindi cha miaka mingine mitano, na kudumisha mamlaka ya Marekani ya kuendelea kuiwekea Tehran vikwazo vya kiuchumi.

    Maelezo zaidi:

  4. Tetesi za Soka: Manchester United yamtupia jicho Branthwaite

    Manchester United wanaendelea kufuatilia kiwango cha beki wa Everton na timu ya taifa ya England, Jarrad Branthwaite, huku wakitathmini uwezekano wa kumsajili mlinzi huyo mwenye umri wa miaka 24. (Football Insider)

    Tottenham Hotspur wanko kifua mbele katika mbio za kuwania saini ya beki chipukizi wa Brazil, Arthur Dias, anayekipiga Athletico Paranaense. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 pia anawindwa na Newcastle United, Nottingham Forest na Brentford, huku akitajwa kuwa na thamani ya euro milioni 30. (Teamtalk)

    Monaco wameweka wazi mipango ya kumuuza mshambuliaji wa Marekani, Folarin Balogun, katika dirisha la usajili la Januari. Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 kubatilisha mpango wake wa kuhamia Everton siku ya mwisho ya dirisha la usajili. (Standard)

    Vilabu kadhaa barani Ulaya vinaendelea kufuatilia hali ya beki kijana wa Chelsea, Josh Acheampong. Mlinzi huyo wa England mwenye umri wa miaka 20 ameibua kuvutia kwa timu mbalimbali zinazotaka kupata huduma zake. (Standard)

    Pia unaweza kusoma:

    Klabu ya Monaco imedokeza kuwa kiungo wa Senegal Lamine Camara, 22, anaweza kuondoka katika dirisha la usajili la Januari, huku Liverpool na Chelsea zikitajwa kuwania saini yake. (Standard)

    Real Madrid inajiandaa kufanya kila iwezalo kumsajili kiungo chipukizi wa Morocco, Abdellah Ouazane, aliye na umri wa miaka 17, anayekipiga Ajax. (Fichajes - kwa Kihispania)

    Newcastle United wanatarajiwa kurejesha nia yao ya kumsajili kiungo wa Djurgarden, Bo Hegland, baada ya mchezaji huyo wa Norway mwenye umri wa miaka 22 kukataa kuhamia klabu hiyo wakati wa dirisha la usajili la majira ya joto. (Football Insider)

    Arsenal, Brighton na Aston Villa wanaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya kiungo wa Sturm Graz, Luca Weinhandl, mwenye umri wa miaka 17. Mchezaji huyo wa Austria anakadiriwa kuwa na thamani ya pauni milioni 20.

    Tottenham Hotspur wanafikiria kumsajili mshambuliaji raia wa Argentina Mauro Icardi kwa uhamisho wa bure baada ya kuondoka Galatasaray. Hata hivyo, klabu hiyo haitamruhusu kusajiliwa rasmi hadi dirisha la Januari kutokana na kanuni za usajili.

    Man City na Liverpool wamuwania Nmecha

    Manchester City na Liverpool zimeonyesha nia ya kumsajili kiungo wa kimataifa wa Ujerumani Felix Nmecha, mwenye umri wa miaka 25. Borussia Dortmund inadaiwa kutaka kati ya euro milioni 80 na 90 ili kumuachia mchezaji huyo.

    Chelsea yaingia mbio za kumwania Adama Jeng

    Chelsea imejiunga na vilabu kadhaa vya Ulaya vinavyowania saini ya nyota chipukizi wa Gambia, Adama Jeng, mwenye umri wa miaka 15, ambaye kwa sasa anachezea klabu ya Norway ya Tromso IL.

  5. Saudi Arabia yatoa tahadhari ya mashambulizi ya anga mjini Riyadh

    Wakazi wa mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, wamearifiwa kuwa hali ya usalama imerejea kuwa ya kawaida baada ya mamlaka kutoa tahadhari za mashambulizi ya anga kufuatia taarifa za milipuko kusikika katika jiji hilo.

    Hii ni mara ya kwanza kwa tahadhari za mashambulizi ya anga kutolewa mjini Riyadh tangu Wahouthi waongeze mashambulizi yao na kutangaza kile walichokiita “mzingiro wa baharini” dhidi ya Saudi Arabia mwezi Julai.

    Mamlaka ya Ulinzi wa Kiraia ya Saudi Arabia ilitoa tahadhari hizo kwa wakazi wa Riyadh na maeneo mengine kadhaa usiku wa kuamkia Jumamosi, huku mvutano kati ya ufalme huo na Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran ukiendelea kuongezeka.

    Waandishi wa mashirika ya habari ya Reuters na AFP waliripoti kusikia milipuko katika mji mkuu huo. Hata hivyo, mamlaka baadaye zilithibitisha kuwa hatari ilikuwa imedhibitiwa na kuwashauri wananchi kujiepuka na mikusanyiko mikubwa ya watu hadi hali itakapotulia kikamilifu.

    Katika siku za karibuni, Wahouthi walitangaza kuteka mji wa bandari wa Mokha pamoja na Kisiwa cha Perim, maeneo yenye umuhimu mkubwa wa kimkakati katika njia ya usafiri wa baharini inayotumiwa na Saudi Arabia kusafirisha mafuta na bidhaa kuelekea masoko ya Asia na Ulaya.

    Msemaji wa kijeshi wa Wahouthi amesema hatua ya kundi hilo kuweka kizuizi cha baharini ni jibu kwa kile walichokitaja kuwa vikwazo vya Saudi Arabia dhidi ya bandari na viwanja vya ndege vilivyoko katika maeneo ya Yemen yanayodhibitiwa na Wahouthi.

    Saudi Arabia imekuwa ikitegemea kwa kiasi kikubwa njia ya Bahari ya Shamu kwa usafirishaji wa mafuta yake tangu usafiri kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz uathiriwe na mivutano ya kikanda.

    Wiki iliyopita, Wahouthi walidai kufanya mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya miundombinu kadhaa ya mafuta ya Saudi Arabia.

    Mashambulizi hayo yalisababisha moto katika baadhi ya maeneo na kuathiri kwa muda shughuli za uzalishaji.

    Maelezo zaidi:

  6. Marekani na Denmark zafikia makubaliano kuhusu Greenland baada ya vitisho vya Trump

    Marekani na Denmark zimefikia makubaliano kuhusu usalama wa Greenland, hatua inayotarajiwa kumaliza mvutano wa kidiplomasia uliodumu kwa miezi kadhaa kufuatia matamshi ya Rais Donald Trump kuhusu kulitaka eneo hilo kwa misingi ya usalama wa taifa.

    Trump alisema makubaliano hayo yataipa Marekani "udhibiti wa kudumu wa masuala ya usalama na mahitaji mengine yote" katika Greenland, eneo la Denmark lenye mamlaka ya ndani.

    Viongozi wa Denmark na Greenland wamekaribisha makubaliano hayo, wakisema yatasaidia kuimarisha usalama wa eneo hilo. Hata hivyo, hawajafichua maelezo ya makubaliano hayo, ambayo yanatarajiwa kutiwa saini wiki ijayo.

    Tangazo hilo linafuatia miezi kadhaa ya matamshi ya Rais Donald Trump kuhusu kutaka kuipata Greenland, akisisitiza umuhimu wake wa kimkakati katika masuala ya ulinzi pamoja na utajiri wake mkubwa wa rasilimali za madini.

    Maudhui kamili ya makubaliano hayo bado hayajawekwa wazi. Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema makubaliano hayo hayataigharimu Marekani chochote na yataipa mamlaka ya kuchukua hatua zote zitakazoonekana muhimu kwa ajili ya kulinda na kuimarisha usalama wa Greenland.

    Kwa mujibu wa Trump, makubaliano hayo pia yanazuia nchi au makundi yanayochukuliwa kuwa maadui wa Marekani kuwa na uwepo wa kijeshi Greenland au kuwekeza katika miradi nyeti bila idhini ya wazi ya Washington.

    Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, alisema ana matumaini kwamba makubaliano hayo yatakuwa na manufaa kwa Denmark, Greenland na Marekani. Yanatarajiwa kutiwa saini pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wiki ijayo.

    Katika taarifa ya pamoja na Waziri Mkuu wa Greenland, Jens-Frederik Nielsen, Frederiksen alisema makubaliano hayo yataimarisha usalama wa pamoja katika eneo la Aktiki na Atlantiki ya Kaskazini, huku yakiheshimu mamlaka ya Denmark na kulinda haki ya wananchi wa Greenland kujiamulia mustakabali wao.

    Soma zaidi:

  7. Trump apiga marufuku CNN na Politico White House

    Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa CNN, MSNBC na Politico hazitaruhusiwa kuingia White House, katika kile kinachoonekana kuwa hatua mpya ya mzozo wake wa muda mrefu na vyombo vya habari.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social siku ya Ijumaa, Trump alidai kuwa vyombo hivyo mara kwa mara huchapisha au kuripoti taarifa za uongo kuhusu utawala wake, ingawa hakutoa mifano ya madai hayo.

    Baadaye, Trump alielezea hatua hiyo kama “marufuku rahisi sana”, lakini hakufafanua namna ambavyo itatekelezwa kwa vitendo. Kufikia sasa, haijafahamika wazi iwapo waandishi na wafanyakazi wa vyombo hivyo watazuiwa kuingia katika eneo la Ikulu ya White House.

    CNN imekosoa vikali tangazo hilo, ikilitaja kuwa “shambulio lisilo halali” dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Marekani. Hatua hiyo pia inatarajiwa kukabiliwa na changamoto za kisheria.

    Muda mfupi baada ya tangazo la Trump, waandishi wa habari wa CNN na Politico walikuwa bado wakifanya kazi ndani ya eneo la White House.

    Wakati huo huo, timu ya CNN iliendelea kuandamana na Makamu wa Rais JD Vance katika safari yake ya kuhudhuria hafla moja katika jimbo la Iowa.

    Katika taarifa yake, CNN ilisema marufuku hiyo i haina msingi wa kisheria na kusisitiza kuwa inaunga mkono kikamilifu timu yake ya waandishi wa habari wa White House pamoja na taarifa zao ambazo imezitaja kuwa za haki na sahihi.

    Nayo Politico ilisema itaendelea kuripoti shughuli za Ikulu ya White House kwa usawa na bila upendeleo.

    “Tutaendelea kuripoti kwa haki kuhusu White House ya sasa na tawala zitakazofuata,” ilisema katika taarifa yake.

    “Tutazitetea kwa nguvu zote haki zetu chini ya Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Marekani dhidi ya jaribio lolote la kuzikiuka.”

    MS NOW, ambayo hapo awali ilijulikana kama MSNBC, ilikataa kutoa maoni kuhusu tangazo hilo.

    Tangu kurejea madarakani mwezi Januari 2025, Rais Donald Trump na maafisa wa utawala wake wamekuwa katika mivutano ya mara kwa mara na wanahabari wanaoripoti shughuli za Ikulu ya White House.

    Katika muhula wake wa pili, Trump pia amepanua wigo wa vyombo vinavyopata fursa ya kuripoti kutoka White House kwa kuwakaribisha wanablogu wenye misimamo ya kihafidhina, watu wenye ushawishi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari visivyo vya kawaida.

    Utawala wake umesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha umma wa Marekani unapata mitazamo mbalimbali na sauti tofauti katika uwasilishaji wa habari kutoka Ikulu ya White House.

    Maelezo zaidi:

  8. Natumai hujambo. Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.