Serikali ya Kenya yasema haijapokea taarifa rasmi kuhusu madai ya kutekwa kwa Twaha Mwaipaya
Ofisi ya Msemaji wa Serikali ya Kenya imesema haijapokea taarifa rasmi kutoka kwa taasisi yoyote kuhusu raia wa Tanzania, Twaha Mwaipaya, anayedaiwa kutekwa nchini humo.
“Bado hatujapata taarifa kuhusu tukio hilo, hivyo tunalifuatilia,” ofisi hiyo imeiambia BBC Swahili.
Kauli hiyo inakuja baada ya Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya pia kusema kuwa haujapokea taarifa zozote kuhusu madai ya kutekwa kwa mwanaharakati huyo.
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International Kenya liliripoti tukio hilo, likisema Mwaipaya alizuiliwa na watu waliokuwa wakitumia magari matatu, likiwamo Toyota Land Cruiser Hardtop.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii Jumapili, shirika hilo lilisema Mwaipaya, raia wa Tanzania, alidaiwa kutekwa majira ya saa nane mchana katika eneo la Kamulu, Kaunti ya Machakos.
“Alikuwa akisafiri kwa teksi kwenda kuwatembelea marafiki,” ilisema taarifa hiyo.
Mashirika ya haki za binadamu, yakiwemo Amnesty International Kenya na Defenders Coalition, yametaka hatua za haraka zichukuliwe kumtafuta.
Kisa hicho pia kimeibua upya wasiwasi kuhusu kile ambacho mashirika hayo yanakitaja kuwa ukandamizaji unaovuka mipaka ya nchi dhidi ya wapinzani wa kisiasa na watetezi wa haki za binadamu.
Kwa upande wake, serikali ya Tanzania imekuwa ikikanusha madai ya kuhusika na vitendo visivyo halali dhidi ya wapinzani wa kisiasa.
Hadi kufikia sasa, hakuna taarifa rasmi au tamko lolote lililotolewa na mamlaka za usalama nchini Kenya kuhusiana na tukio hilo la kutekwa kwa Mwaipaya.
BBC Swahili inaendelea kufuatilia suala hilo na kutafuta ufafanuzi kutoka kwa mamlaka husika nchini Kenya, ikiwamo ofisi inayoshughulikia masuala ya nje.