Marekani yafanya mashambulizi mapya; Iran yafunga mlango wa bahari wa Hormuz
Marekani imesema imeanzisha wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya Iran baada ya Iran kushambulia meli iliyokuwa ikipita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) limetangaza kufungwa kwa njia hiyo muhimu ya baharini hadi itakapotolewa taarifa nyingine, huku likionya kuhusu hatua kali dhidi ya kile lilichokiita "uchokozi" wa Marekani, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.
Saa chache baada ya mashambulizi ya Marekani, IRGC ilidai kuwa imelenga kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Jordan. Wakati huo huo, Falme za Kiarabu (UAE), Qatar na Bahrain ziliripoti kuchukua hatua za kukabiliana na makombora na ndege zisizo na rubani zilizorushwa kutoka Iran.
Mvutano huo unafuatia matukio ya mapema wiki hii ambapo meli tatu za kibiashara za kubeba mafuta zilishambuliwa, hali iliyosababisha mashambulizi ya kulipizana kisasi kati ya Marekani na Iran.
Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema imeanzisha duru ya tatu ya mashambulizi wiki hii baada ya IRGC kushambulia "waziwazi" meli yenye usajili wa Cyprus, MV GFS Galaxy, iliyokuwa ikivuka Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Kwa mujibu wa CENTCOM, meli hiyo iliharibiwa vibaya katika chumba cha injini na haikuweza kuendelea na safari yake. Aidha, mfanyakazi mmoja wa kiraia wa meli hiyo anaripotiwa kutojulikana alipo.
Shirika la Uingereza la UK Maritime Trade Operations (UKMTO) limesema lilifahamishwa na mamlaka za kijeshi kuwa wafanyakazi wa meli walilazimika kuiacha baada ya kushambuliwa na kuanza kutumia boti ya kujiokoa.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, CENTCOM ilisema Iran ilipewa fursa nyingine ya kuonyesha kwamba inazingatia makubaliano ya Maelewano baada ya kuwajibishwa kwa mashambulizi ya awali dhidi ya meli za kibiashara, lakini "imeshindwa kufanya hivyo kwa mara nyingine."
Soma Zaidi Hapa: