Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Eritrea: Waziri wa zamani afariki jela baada ya miaka sita bila kufunguliwa mashtaka

Waziri wa zamani wa fedha wa Eritrea na mkosoaji mkali wa rais wa nchi hiyo - Berhane Abrehe - amefariki akiwa gerezani, familia yake imesema.

Muhtasari

  • Tanzania: Wakazi wa Ngorongoro kushiriki shughuli zote za uchaguzi
  • Maafisa wanne wauawa baada ya wafungwa kuasi katika gereza la Urusi
  • Manchester City yamsajili tena Gundogan kutoka Barcelona
  • Homa ya Nyani: Kenya yathibitisha mgonjwa wake wa pili
  • Macron akutana na viongozi wa kisiasa katika juhudi ya kumtafuta Waziri Mkuu
  • Taiwan yawafunga maafisa wake kwa kufanyia ujasusi China
  • Mikoa ya Ukraine yashambuliwa na ndege zisizo na rubani za Urusi - Vikosi vya Ukraine
  • BBC imemfuta kazi mtangazaji Jermaine Jenas baada ya malalamiko
  • Democrat wakataa ombi la waandamanaji wa Gaza la kutoa nafasi ya kuzungumza kwa Wapalestina
  • Rwanda yasimamisha utendaji wa mashirika 43 ya kidini kwa ukiukaji wa sheria
  • Vita vya Ukraine: Feri ya reli yazama katika bandari Urusi baada ya shambulio la Wanajeshi wa Ukraine
  • Democrat wakataa madai ya waandamanaji wa Gaza kutoa nafasi ya kuzungumza kwa Wapalestina
  • Vita vya Ukraine: Feri ya reli yazama katika bandari Urusi baada ya shambulio la Wanajeshi wa Ukraine
  • Uchaguzi wa Marekani 2024: Harris aapa kutoa fursa ‘mpya ya kusonga mbele ’ kwa Wamarekani huku akikubali uteuzi wake
  • Wafanyabiashara wa silaha wa Yemen wanauza silaha kwenye X

Moja kwa moja

Na Dinah Gahamanyi & Ambia Hirsi

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Tanzania: Wakazi wa Ngorongoro wahakikishiwa kushiriki shughuli zote za uchaguzi

    Rais wa wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro kuwa shughuli zote za uchaguzi wa serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 pamoja na Uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 zitaendelea kama ilivyokuwa awali, amesema Waziri katika Waziri Mkuu William Lukuvi.

    Bw Lukuvi ametoa kauli hiyo leo Ijumaa alipozungumza na mamia ya wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro akiongeza kuwa uchaguzi huo utazingatia taratibu na mipaka ya vijiji na vitongoji iliyokuwepo awali kwenye maeneo ya wilaya hiyo.

    ''Rais Samia bado anatambua uwepo wa serikali za vijiji na vitongoji vya maeneo hayo'' alisema,

    Pia amewataka askari wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kutowanyanyasa wananchi pamoja na kuheshimu mamlaka za serikali za mitaa zilizopo.

    Kwa upande wake Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amemhakikishia Waziri Lukuvi kuwa atasimamia maelekezo yote yaliyotolewa kwake.

    Katika ziara hiyo, Waziri Lukuvi ameambatana na Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi Waziri wa Katiba na sheria, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dunstan Kitandula pamoja na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania CP Awadh Juma Haji pamoja na Viongozi wengine wa serikali na wa Chama Cha Mapinduzi CCM.

  3. Maafisa wanne wauawa baada ya wafungwa kuasi katika gereza la Urusi

    Wafanyakazi wanne wa magereza wameuawa baada ya wafungwa kufanya uasi katika jela la Urusi na kushikilia mateka kadhaa,mamlaka inasema.

    Vikosi maalum vilivamia kituo cha IK-19 cha Surovikino katika eneo la kusini-magharibi mwa mkoa wa Volgograd baada ya wafungwa waliokuwa na visu, waliojitambulisha kuwa wanamgambo wa Islamic State (IS) kudai kuwa wamechukua udhibiti wa jengo hilo.

    Mamlaka zilisema operesheni hiyo ya kikosi maalum imefanikiwa kuwakomboa baadhi ya mateka "kuwadhibiti" washambuliaji wote, lakini baadaye walithibitisha kuwa wafanyikazi wanne wa magereza walikufa katika shambulio hilo.

    Picha ambayo haijathibitishwa iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii ilionekana kuonyesha mfungwa aliyeshikilia kisu akimkanyagia chini mlinzi wa gereza aliyekuwa ikivuja damu wakati wa uasi huo.

    Gavana wa mkoa wa Volgograd Andrei Bocharov alisema mapema kwamba utekaji nyara huo "hakuna tishio kwa raia".

    Rais Vladimir Putin alirekodiwa akishiriki katika mkutano na wakuu wa usalama, wakati ambapo Kremlin ilisema amedhibiti hali hiyo.

    Hii ni mara ya pili kwa tukio kama hilo kutokea katika Utekaji huko Volgograd msimu huu wa wa majira ya joto, baada ya wafungwa sita waliodai kuwa watiifu kwa kundi la Islamic State kuwakamata walinzi wawili katika kituo kimoja katika eneo jirani la Rostov.

    Wafungwa watano kati ya hao waliuawa na wa sita kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kufuatia shambulio hilo.

  4. Eritrea: Waziri wa zamani afariki jela baada ya miaka sita bila kufunguliwa mashtaka

    Waziri wa zamani wa fedha wa Eritrea na mkosoaji mkali wa rais wa nchi hiyo - Berhane Abrehe - amefariki akiwa gerezani, familia yake imesema.

    Mzee huyo mwenye umri wa miaka 79 alikuwa waziri wa fedha aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi Eritrea, lakini aliondolewa katika nafasi yake mwaka 2012 baada ya kutofautiana na Rais Isaias Afwerki.

    Miaka sita baadaye, alifungwa jela baada ya kuchapisha kitabu kinachomueleza rais kuwa ni “dikteta” anayetakiwa kujiuzulu.

    Familia yake iliambia BBC kwamba mamlaka, ambayo huthibitisha vifo vya maafisa wakuu waliokuwa kizuizini imewaarifu kuhusu kifo cha Bw Berhane.

    Serikali pia hushiriki mara chache mahali miili hiyo huzikwa lakini familia ya Bw Berhane imesikia kuna mpango wa kumzika katika makaburi ya Asmara Patriots.

    Ni maveterani pekee wa vita vya uhuru wa Eritrea, kama Bw Berhane, au wanachama wa huduma ya kitaifa ndio wanaoweza kuzikwa hapo.

    Mwili wake bado haujaachiliwa, familia yake ilisema, na haijabainika hasa Bw Berhane alifariki lini na kifo chake kilisababishwa na nini.

    Rais Isaias ameiongoza nchi hiyo ya Afrika Mashariki, bila kufanya uchaguzi wa kitaifa, tangu kushinda vita vya uhuru dhidi ya Ethiopia mwaka 1991.

  5. Manchester City yamsajili tena Gundogan kutoka Barcelona

    Manchester City wamekamilisha usajili wa nahodha wa zamani Ilkay Gundogan kutoka Barcelona kwa mkataba wa awali wa mwaka mmoja na chaguo la miezi 12 zaidi.

    Kiungo huyo wa kati wa Ujerumani, ambaye alikuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na Pep Guardiola katika klabu hiyo mwaka 2016, alichezea City kwa miaka saba kabla ya kujiunga na Barcelona kwa uhamisho wa bure mwaka 2023.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 alishinda mataji 14 katika kipindi chake cha kwanza Etihad, akifunga mabao 60 katika mechi 304.

    "Kila mtu anajua heshima niliyo nayo kwa Pep - ni kocha bora zaidi duniani na kufanya kazi naye kila siku kunakufanya kuwa mchezaji bora. "Kusema kweli, nakamia kuvaa tena jezi ya City," Gundogan alisema.

  6. Homa ya Nyani: Kenya yathibitisha mgonjwa wake wa pili

    Wizara ya afya ya Kenya inasema mwanamume ambaye ni dereva wa lori mwenye historia ya kusafiri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (D.R.C.) amepatikana na virusi vya Homa ya Nyani au Mpox.

    Derva huyo alifanyikwa uchunguzwa katika mji wa mpakani wa Busia magharibi mwa Kenya.

    Sampuli yake ilithibitishwa kuwa na virusi katika uchubguzi wa maabara. Mtu huyo kwa sasa ametengwa na yuko chini ya uangalizi wa karibu.

    Aidha uchunguzi wa kina wa watu wanaoshukiwa kuwa na virusi vya Mpox umeimarishwa katika eneo hilo na katika kaunti zote ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

  7. Ufaransa: Macron akutana na viongozi wa kisiasa katika juhudi ya kumtafuta Waziri Mkuu

    Rais Emmanuel Macron leo (Ijumaa) amekutana na viongozi wa mrengo wa kushoto kwa mazungumzo ya siku mbili yaliyolenga kuamua nani ataunda serikali ijayo ya Ufaransa.

    Uchaguzi wa mapema uliofanyika Julai ulisababisha mkwamo katika siasa za Ufaransa chama chochote kilichoweza kupata wingi wa wazi katika Bunge la Kitaifa.

    Serikali ya muda iliongoza Ufaransa wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Paris, kwa hasira ya muungano wa mrengo wa kushoto ambao uliongoza uchaguzi huo.

    Chama chao cha New Popular Front cha vyama vinne kinataka mtumishi mkuu wa serikali asiyejulikana sana aitwaye Lucie Castets kuteuliwa kuwa waziri mkuu.

    Hata hivyo, mwanauchumi huyo mwenye umri wa miaka 37 hajachaguliwa na anaonekana kama chaguo la urais kwa waziri mkuu.

  8. Taiwan yawafunga maafisa wake kwa kufanyia ujasusi China

    Mahakama moja mjini Taipei imewafunga jela wanajeshi wanane wa Taiwan kwa kufanya ujasusi kwa niaba ya China ili wapate pesa.

    Maafisa wa kijeshi waliostaafu waliwahonga askari waliokuwa kazini dola 21,900 za Kimarekani ili wajiunge na mtandao wa kijasusi, mahakama ilibaini.

    Mmoja wa watu hao, ambaye aliaminika kuwa muhimu katika kuwasajili wanajeshi, alihukumiwa kifungo cha miaka 13 gerezani.

    Mmoja wa wanajeshi hao, Luteni Kanali, alihukumiwa kifungo cha miaka tisa kwa kupanga kuhamia China kwa kuruka kutoka kwenye helikopta, huku mwingine akipiga video ya mafundisho kuhusu kujisalimisha kwa China katika tukio la vita.

    China inaichukulia Taiwan inayojitawala kama jimbo lake lililojitenga na ambalo hatimaye litakuwa chini ya udhibiti wake, imekuwa ikifanya kila juhudi kuchukua kisiwa hicho.

    Pande hizo mbili zimekuwa zikifanya ujasusi tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya China mwaka 1949.

    Watu kumi walishtakiwa kwa ujasusi mwaka jana, na wanane kati yao walihukumiwa siku ya Alhamisi.

  9. Mikoa ya Ukraine yashambuliwa na ndege zisizo na rubani za Urusi - Vikosi vya Ukraine

    Jeshi la anga la Ukraine linaonya kuwa maeneo kadhaa ya Ukraine yanashambuliwa na ndege zisizo na rubani za Urusi.

    Kwa mujibu wa jeshi la Ukraine, kundi la ndege zisizo na rubani za Shahed zilionekana katika eneo la Sumy na sasa zinaelekea katika mkoa wa Poltava. Jeshi la Kiukreni linazungumzia juu ya hatari ya mashambulizi huko Myrhorod.

    Aidha, droni zinazoongozwa kufanya mashambulizi zimekuwa zikitoka mkoa wa Kherson kuelekea maeneo ya Mykolaiv.

    Pia kuna hatari ya mashambulizi katika mikoa ya Kirovograd na Cherkasy, Jeshi la Anga la Ukraine limeandika kwenye kituo chake cha Telegram.

    Wakati huo huo shirika la habari la Marekani la Associated Press linaripoti, likinukuu vyanzo vyake, kwamba utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden hivi karibuni utaipatia Ukraine msaada mpya wa kijeshi wenye thamani ya dola milioni 125.

    Kwa mujibu wa shirika hilo, msaada huo utajumuisha risasi kwa ajili ya mifumo ya roketi ya ufyatuaji ya HIMARS, makombora mbalimbali ya kupambana na vifaru, ikiwa ni pamoja na Javelin, mifumo ya kukabiliana na droni na mifumo ya vita vya elektroniki, pamoja na makombora ya 155- na 105-millimeter.

    Kama ilivyoelezwa katika chapisho hilo, Ikulu ya White House inaweza kutangaza rasmi mpango huo mpya mapema Ijumaa.

    Silaha hizo zitatumwa chini ya mpango wa rais (PDA), ikimaanisha kuwa zitapelekwa Ukraine haraka moja kwa moja kutoka kwenye ghala za silaha za Pentagon.

    Shirika la habari la Associated Press linakadiria kuwa kuidhinishwa kwa msada wa hivi karibuni kutaifanya thamani ya jumla ya misaada ya kijeshi ya Marekani iliyotolewa kwa Kyiv tangu kuanza kwa uvamizi kamili wa Urusi kufikia hadi dola bilioni 55.7.

    Soma zaidi:

  10. BBC imemfuta kazi mtangazaji Jermaine Jenas baada ya malalamiko

    Jermaine Jenas, mchezaji wa zamani wa soka ambaye ni mtangazaji katika kipindi cha The One Show na kuonekana kwenye Match of the Day kwa BBC, amefutwa kazi na shirika hilo kufuatia malalamiko kuhusu tabia yake kazini.

    Jenas mwenye umri wa miaka 41, ameondolewa kutangaza kwenye vipindi viwili muhimu.

    BBC News inaelewa kuwa mkataba wake ulikatishwa wiki hii kwa sababu ya masuala yanayodaiwa kuhusiana na tabia kazini.

    Akijibu habari hizo, Jenas alisema kuna "pande mbili kwa kila habari" lakini atawaacha "wanasheria wake washughulikie suala hilo".

    Madai hayo yanahusisha mawasiliano ya kidijitali kama vile maandishi, ambayo yalitolewa na shirika hilo wiki chache zilizopita.

    Katika mahojiano na radio talkSport, alisema mara kwa mara "Siwezi kuzungumza juu yake" alipoulizwa juu ya madai hayo.

    "Mimi, kama unavyoona, sifurahii suala hilo," aliambia kituo hicho.

    Alipoulizwa kama alishangazwa na malalamiko yoyote dhidi yake, Jenas alisema tena: "Siwezi kuzungumza kwa sasa."

    "Lazima niiachie timu ya mawakili kwa sasa ambao ni, ndio, nadhani wanashughulikia hali hiyo," alisema.

    "Hii ni..., ni ngumu, unajua. Lakini sina budi kuwasikiliza mawakili wangu.

    "Msemaji wa BBC alisema: "Tunaweza kuthibitisha Jermaine Jenas si sehemu yetu ya watangazaji."

    Alikuwa hewani mara ya mwisho kwa shirika hilo mapema wakati wa msimu wa kiangazi.

    Jenas, ambaye ameoa na ana watoto wanne, alipata mshahara wa kati ya £190,000 - £194,999 katika idhaa BBC kwa kazi yake ya Kombe la FA, Mechi Bora ya Siku na Kombe la Dunia.

  11. Democrat wakataa ombi la waandamanaji wa Gaza la kutoa nafasi ya kuzungumza kwa Wapalestina

    Wademocrat wamekataa matakwa ya waandamanaji kumruhusu Mpalestina kuzungumza katika Kongamano la Kitaifa la Democrat lililofanyka Chicago.

    Wajumbe wa chama hicho ambao wanaopinga uungaji mkono wa Marekani wa vita vya Israel huko Gaza - walianza mgomo wa kukaa nje ya milango ya uwanja Jumatano usiku.

    Lakini kufikia saa kumi na mbili jioni kwa saa za eneo siku ya Alhamisi - muda wa mwisho wa waandamanaji walikuwa wanatumaini kusikia kutoka kwa jibu kutoka kwa kampeni ya Kamala Harris - wanaharakati walisema hawajapata jibu la maombi yao ya kuruhusiwa kwa Mpalestina kupanda jukwaani.

    Mgomo wa kukaa ndani usiku wa mwisho wa mkutano huo yalikuja wakati maelfu ya waandamanaji nje ya eneo wakiendelea kupinga vita vya Gaza na sera ya White House.

    Maandamano hayo wiki hii yamekuwa ya amani kwa kiasi kikubwa, isipokuwa maandamano madogo, yasiyo na kibali nje ya ubalozi mdogo wa Israel ambayo yalisababisha kukamatwa kwa watu 56 .

    "Huu umekuwa uamuzi mbaya wa uongozi wa Kidemokrasia kukataa ombi la chini kabisa ambalo tuliomba wiki zilizopita, kabla ya kongamano," alisema Layla Elabed, kiongozi mwenza wa vuguvugu la kitaifa lisilo na nia.

    Afisa wa kampeni ya Harris iliiambia BBC kwamba meneja wa kampeni Julie Chavez Rodriguez alikutana na viongozi kutoka vuguvugu hilo hivi karibuni.

  12. Rwanda yasimamisha utendaji wa mashirika 43 ya kidini kwa ukiukaji wa sheria

    Serikali ya Rwanda imetoa orodha ya majina ya mashirika ya kidini yaliyopigwa marufuku kwa kukiuka sheria. Orodha hiyo inajumuisha mashirika 43 ambayo yamekuwa yakiendesha shughuli zake katika wilaya 18 kote nchini Rwanda.

    Hatua hii imefuatia shughuli za uchunguzi unaoendelea wa utendaji wamashirika yenye misingi ya imani ulioanza tarehe 28 Julai.

    Tangu mwezi Julai Rwanda imefunga makanisa 4,000 katika kipindi cha mwezi kwa kushindwa kuzingatia kanuni za afya na usalama, ikiwa ni pamoja na kutozuiliwa ipasavyo.

    Hatua hiyo iliathiri zaidi makanisa madogo ya Kipentekoste – ambayo baadhi yaliendesha ibada nje ya mapango au kwenye kingo za mito.

    "Hii haifanywi kuwazuia watu kusali bali kuhakikisha usalama na utulivu wa waumini," Waziri wa Serikali ya Mitaa Jean Claude Musabyimana aliviambia vyombo vya habari vya serikali.

    Ni msako wa kwanza mkubwa tangu sheria ilipobuniwa miaka mitano iliyopita kudhibiti maeneo ya ibada.

    Sheria kuhusu Imani inayataka makanisha kuendesha ibada kwa mpangilio katika mazingira salama na vile vile kuharamisha matumizi yao vipaza sauti.

    Sheria hiyo pia inawalazimu wahubiri wote kupata mafunzo ya kidini kabla ya kufungua kanisa.

    Sheria ilipopitishwa mwaka wa 2018 takriban makanisa 700 yalifungwa hapo awali.

    Wakati huo, Rais wa Rwanda Paul Kagame alisema nchi hiyo haihitaji nyumba nyingi za ibada, akishikilia kuwa idadi hiyo kubwa inafaa tu kwa uchumi ulioendelea zaidi na njia za kuziendeleza.

    Mengine ni makubwa, yanavutia maelfu ya waumini kila Jumapili, lakini mengine ni majengo madogo yaliyojengwa bila idhini.

  13. Vita vya Ukraine: Feri ya reli yazama katika bandari Urusi baada ya shambulio la Wanajeshi wa Ukraine

    Ukraine imeishambulia feri ya reli yenye matanki ya mafuta kwenye bandari ya Kavkaz katika eneo la Krasnodar baada ya moto kutokea, ilizama chini.

    Siku ya Alhamisi alasiri, chaneli za telegraph ziliripoti shambulio la makombora katika eneo la bandari ya Kavkaz habari hiyo imethibishwa na viongozi wa eneo hilo.

    Bandari "Kavkaz" ni bandari ya pili katika suala la mauzo ya mizigo katika bonde la Bahari Nyeusi-Azov baada ya bandari ya Novorossiysk. Iko katika eneo la Kerch Strait, ambalo linaitenganisha Crimea, iliyounganishwa na Urusi, kutoka eneo la bara.

    Kulingana na makao makuu ya operesheni ya mkoa, moto ulianza kwenye kivuko kutokana na shambulizi.

    Makao makuu ya operesheni ya kikanda yametaja shambulio hilo la wanajeshi wa Ukraine kama "jaribio jingine la shambulio la kigaidi."

    Telegramu za mitaa na kurasa za umma zilichapisha picha ambazo zilionyesha moshi mkubwa ukitoka kwenye kivuko kinachowaka ukionekana juu ya bandari ya Kavkaz.

    Soma zaidi:

  14. Uchaguzi wa Marekani 2024: Harris aapa kutoa fursa ‘mpya ya kusonga mbele ’ kwa Wamarekani huku akikubali uteuzi wake

    Kamala Harris amekubali rasmi uteuzi wake kama mgombea wa urais wa chama cha Democrat katika kongamano la kitaifa la chama hicho.

    Mgombea huo ameahidi kuongoza kwa ajili ya Wamarekani wote alipokuwa akitoa hotuba kuhusu uchaguzi kwa mamilioni ya Wademocrat iliyokamilisha kongamano la kitaifa la chama hicho.

    Bi Harris amezungumzia masuala mbalimbali ya kitaifa ambapo kuhusu usalama wa mpaka, ambalo Republican wamekuwa wakitumia kumshambulia mgombea huyo wa Democratic.

    Akizungumzia kuhusu mustakabal wa Marekani Bi Harris amesema:

    "Ninaipenda nchi yetu kwa moyo wangu wote. Popote ninapoenda na kila mtu ninayekutana naye, naona taifa ambalo liko tayari kusonga mbele, tayari kwa hatua inayofuata na safari ya ajabu ya Marekani," anasema.

    Amesema Wamarekani wana mengi zaidi sawa kuliko yale yanayowagawanya.

    "Hakuna hata mmoja wetu anayepaswa kushindwa ili sisi sote tufanikiwe," anasema. Anatofautisha hili na kauli ya kampeni ya Trump, ambaye anasema " yuko huko akiidhalilisha Marekani".

    Bi Harris pia amezungumzia kuhusu mswada wa usalama wa mpaka wa pande mbili ambao ulisambaratika katika Bunge la Congress mwaka huu baada ya Trump kuwataka Republican kupiga kura dhidi yake.

    "Donald Trump anaamini kuwa makubaliano ya mpaka yataathiri kampeni yake, kwa hivyo aliamuru washirika wake katika Congress kuua mpango huo," Harris amesema.

    "Sawa nakataa kucheza siasa na usalama wetu."

    Harris anasema anapanga kurudisha mswada huo na kuutia saini kuwa sheria.

    Idadi kubwa ya wahamiaji walizuiliwa kwenye mpaka wakati wa utawala wa Biden-Harris lakini idadi ya vivuko vya wahamiaji visivyo halali sasa imepungua kwa miezi mitano mfululizo.

    Harris amesema kuwa nchi zinazoongozwa na watawala wa kimabavu "zinampigia debe Trump" kwa sababu wanaamini "ni rahisi kudhibiti kwa maneno ya kubembeleza na kupendelea".

    "Wanajua Trump hatawajibisha watawala kwasababu anataka kuwa mbabe mwenyewe," aliuambia umati wa watu waliokuwa wakishangilia.

  15. Wafanyabiashara wa silaha wa Yemen wanauza silaha kwenye X

    Wauzaji wa silaha nchini Yemen wanatumia kwa uwazi mtandao wa kijamii wa X, ambao zamani ulijulikana kama Twitter, kuuza silaha aina ya Kalashnikov, bastola, na guruneti na vilipuzi vya maguruneti.

    Wafanyabiashara hao wanaendesha shughuli zao katika mji mkuu Sana'a na maeneo mengine chini ya udhibiti wa Wahouthi , kundi la waasi linaloungwa mkono na Iran ambalo limepigwa linatambuliwa na Marekani na Australia kama magaidi na kupigwa maruku.

    "Haiwezekani kwamba wao [wachuuzi wa silaha] hawafanyi kazi kwa niaba ya Wahouthi," alisema Balozi wa zamani wa Uingereza nchini Yemen, Edmund Fitton-Brown, ambaye sasa anafanya kazi katika mradi wa kukabiliana na itikadi kali.

    "Wafanyabiashara binafsi ambao walijaribu kufaidika kutokana na kusambaza bidhaa, [kwa mfano] serikali ya Yemen, walizuia haraka."

    Uchunguzi uliofanywa na gazeti la The Times uligundua kuwa akaunti nyingi za Yemen zilikuwa na alama ya uthibitisho.

    The Times na BBC zimetafuta maoni kutoka kwa X kuhusiana na biashara hii , lakini hawajapata jibu lolote hadi sasa.

    Wasimamizi wengi wa maudhui ya jukwaa waliachishwa kazi baada ya mmiliki mpya Elon Musk kununua kampuni hiyo mnamo 2022.

  16. Hujambo na karibu tena kujiunga nasi kwa matangazo yetu ya mubashara ikiwa leo ni tarehe 23.08.2024