Mwaka mmoja bila Raila: Ni nani amenufaika zaidi na pengo aliloacha katika siasa za Kenya?

    • Author, Ambia Hirsi
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Hakuna mwanasiasa mwingine katika historia ya kisasa ya Kenya ambaye ameacha pengo la kisiasa linalozua mjadala mkubwa kama Raila Odinga. Mwaka mmoja baada ya kifo chake, Kenya bado inatafuta jibu la swali ambalo hapo awali lilionekana kuwa gumu hata kulifikiria: ni nani, ikiwa yupo, ameweza kurithi ushawishi wa kisiasa wa mwanasiasa aliyekuwa nguzo kuu ya upinzani kwa zaidi ya miongo mitatu?

Kifo cha Raila mwezi Oktoba 2025 hakikuashiria tu mwisho wa enzi muhimu katika siasa za Kenya, bali pia kilifungua ukurasa mpya wa ushindani kuhusu urithi wake wa kisiasa, msingi wake wa wafuasi na mwelekeo wa harakati alizoziunda kwa miongo kadhaa.

Kwa Wakenya wengi, Raila alikuwa zaidi ya kiongozi wa chama. Alikuwa nembo ya mageuzi ya kidemokrasia, mtetezi wa mabadiliko ya kikatiba na mwanasiasa aliyefaulu mara kwa mara kuunganisha makundi tofauti chini ya ajenda moja ya kisiasa. Ushawishi wake ulivuka mipaka ya ngome yake ya Nyanza na kuenea katika Pwani, Magharibi mwa Kenya, maeneo ya mijini na miongoni mwa vizazi vya wapigakura waliomwona kama sauti ya upinzani na mabadiliko.

Miezi kumi na miwili baadaye, wanasiasa kadhaa wanaonekana kugombea sehemu ya urithi huo. Hata hivyo, kwa mujibu wa mchambuzi wa siasa Calvins Muga, kuna mwanasiasa mmoja ambaye ameonekana kujitokeza zaidi kuliko wengine.

Kupaa kwa Nyota ya Edwin Sifuna

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna ameibuka kuwa mmoja wa viongozi wanaohusishwa zaidi na maadili na misingi ambayo Raila alitetea kwa miaka mingi.

Wakati baadhi ya viongozi wa ODM wakijaribu kufafanua mustakabali wa chama baada ya kifo cha Raila, Sifuna amejijengea taswira ya mtetezi wa siasa za upinzani na kile anachokiita misingi ya awali ya chama hicho.

Kwa mujibu wa Muga, hali hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kukuza hadhi ya kisiasa ya Sifuna.

"Edwin Sifuna ameonyesha kwa kiwango kikubwa kwamba yeye ndiye mwana wa kisiasa wa aliyekuwa Waziri Mkuu," anasema Muga.

Mchambuzi huyo anaamini kuwa Sifuna amefaulu kuendeleza baadhi ya mbinu za kisiasa zilizomtambulisha Raila, zikiwemo uwezo wa kugusa hisia za wananchi kuhusu changamoto zao na kujitokeza kama sauti ya watu wa kawaida.

"Kila somo alilojifunza kutoka kwa aliyekuwa Waziri Mkuu linaonekana wazi. Kwa sasa anayatumia mafunzo hayo kwa vitendo," anasema.

Kupitia jukwaa la Linda Mwananchi, Sifuna amevutia kundi la wafuasi wanaoamini ODM inapaswa kubaki imara kama chama cha upinzani badala ya kusogea karibu zaidi na serikali.

Kwa vijana wengi hasa, mtindo wake wa moja kwa moja na utayari wake wa kuikosoa serikali umempa mvuto mkubwa.

"Anagusa hisia za watu wengi. Kuna wazee, watu wa tabaka la kati na vijana ambao wanaafiki kwa kiasi kikubwa ujumbe anaoutoa," anaongeza Muga.

Hili ni muhimu kwa sababu vijana wanatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuamua mwelekeo wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Wengi wao hawakushuhudia mapambano ya kisiasa yaliyoijenga historia ya Raila, lakini bado wana wasiwasi kuhusu utawala bora, uwajibikaji na fursa za kiuchumi.

Faida ya kisiasa kwa William Ruto

Ingawa Sifuna ameonekana kurithi sehemu ya ufuasi wa Raila, Rais William Ruto anaonekana kuwa mmoja wa walionufaika zaidi na nafasi ya kisiasa iliyoachwa wazi baada ya kifo chake.

Kwa miongo kadhaa, maeneo mengi ya Nyanza na ngome nyingine za ODM yalijengwa kisiasa juu ya uaminifu kwa Raila. Kutokuwepo kwake kumefungua fursa kwa wapinzani wake wa zamani kujaribu kujijenga katika maeneo hayo.

Katika mwaka uliopita, Ruto ameongeza ziara zake katika Nyanza na kuimarisha uhusiano wake na viongozi pamoja na watu wenye ushawishi katika maeneo yaliyokuwa yakichukuliwa kuwa ngome za ODM. Baadhi ya wanafamilia wa Odinga pia wamewahi kupongeza juhudi zake za kushirikiana na viongozi wa eneo hilo.

Hata hivyo, Muga anaonya kuwa kupenya kisiasa katika eneo fulani hakumaanishi moja kwa moja kupata uungwaji mkono wa wapigakura.

"Kupenya katika maeneo hayo ni jambo moja. Lakini mafanikio ya kweli yatapatikana pale wananchi watakapokupigia kura kwa sababu wanakuamini," anasema.

Kwa mtazamo wake, mikutano mikubwa ya kisiasa na ushirikiano na viongozi wa eneo inaweza kuashiria ongezeko la ushawishi, lakini matokeo ya uchaguzi huamuliwa na kura, si umati wa watu pekee.

Kalonzo amekosa fursa?

Baadhi ya wachambuzi walitarajia Kalonzo Musyoka kuibuka kama mrithi wa asili wa nafasi ambayo Raila alikuwa ameijenga ndani ya upinzani.

Akiwa mmoja wa viongozi wakuu wa muungano wa zamani wa Azimio, Kalonzo alionekana kuwa katika nafasi nzuri ya kujaza pengo hilo.

Hata hivyo, Muga anaamini kuwa hajatumia kikamilifu fursa iliyotokana na kuondoka kwa Raila katika ulingo wa siasa.

"Mtu ambaye angeweza kunufaika zaidi kutokana na kutokuwepo kwa aliyekuwa Waziri Mkuu ni Kalonzo," anasema.

Kulingana na yeye, Kalonzo hajajitokeza mara kwa mara katika mijadala ya kitaifa wala kujenga uwepo wa kisiasa unaoweza kulingananishwa na ule ambao Raila aliudumisha kwa miaka mingi kupitia matamko na misimamo yake kuhusu masuala ya kitaifa.

Kutokana na hilo, nafasi hiyo imeanza kuvutia sura nyingine za kisiasa, akiwemo Sifuna.

Vipi kuhusu Gachagua na Joho?

Aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, ameendelea kuimarisha ushawishi wake katika baadhi ya maeneo ya Mlima Kenya. Hata hivyo, Muga anaamini kuwa ukuaji huo hauwezi kuhusishwa moja kwa moja na kutokuwepo kwa Raila.

"Iwe Raila angekuwepo au la, Gachagua bado angeendelea kukua kisiasa katika eneo lake kwa sababu ni mmoja wa viongozi wa Mlima Kenya na ana uwezo wa kuhamasisha watu wake," anasema.

Kwa upande wake, Ali Hassan Joho bado ana ushawishi mkubwa katika Ukanda wa Pwani, lakini hajaonyesha uwezo wa kujenga ushawishi wa kitaifa unaoweza kujaza pengo lililoachwa na Raila.

Tangu ajiunge serikalini, shughuli zake zimeonekana zaidi kuzunguka majukumu yake ya uwaziri kuliko kuongoza harakati pana za upinzani katika ngazi ya kitaifa.

Urithi mkubwa kuliko mtu mmoja

Huenda funzo kubwa zaidi la mwaka uliopita ni kwamba hakuna mwanasiasa aliyefaulu kuchukua nafasi ya Raila Odinga kikamilifu.

Ruto ameongeza fursa zake za kisiasa. Sifuna amepata kasi mpya ya kisiasa. Kalonzo ameendelea kuwa na mwonekano katika siasa za kitaifa. Viongozi wa kikanda nao wameendelea kudumisha ngome zao za jadi.

Lakini ushawishi wa Raila ulijengwa kwa miongo mingi na kuvuka mipaka ya maeneo, makabila na vizazi mbalimbali.

Mwaka mmoja baada ya kifo chake, urithi wake wa kisiasa bado ni eneo la ushindani mkali. Hata hivyo, kwa mujibu wa Muga, ikiwa swali ni nani amenufaika zaidi kutokana na kutokuwepo kwake, jibu lake ni moja.

"Mtu pekee anayebaki katika kundi hilo ni Edwin Watenya Sifuna."

Iwapo kuongezeka kwa ushawishi huo kutamfikisha katika nafasi ya juu zaidi ya uongozi wa kitaifa, hilo linasalia kuwa moja ya maswali makubwa yatakayounda mjadala wa kisiasa nchini Kenya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.