Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Video za mitandao ya kijamii kuhusu usalama wa chakula India zilivyoibua hofu
Ndani ya jiko lake katika mji mkuu wa India, Delhi, Nirmal Rao mwenye umri wa miaka 55 anaweka trei ya manjano yaliyochemshwa ili yakauke kwenye jua la alasiri.
Kwenye kaunta kando yake, anaingiza polepole manjano ya jana iliyokaushwa kwenye mashine ya kuchanganya, akiisaga na kuwa unga laini wa dhahabu.
Hadi hivi karibuni, Rao hakuwahi kufikiria kwamba angetumia jioni yake kusaga viungo nyumbani.
"Hatupaswi kufanya hivi," alisema, akichota unga wa manjano angavu kwenye mtungi. "Lakini huwezi kuamini kile kinachouzwa masokoni tena."
Rao hayuko peke yake. Katika miji yote ya India, baadhi ya familia za tabaka la kati zinabadilisha majiko yao kimya kimya kuwa vitengo vidogo vya kusindika chakula - kusaga viungo kwa mkono, kutengeneza paneer (jibini ya India) nyumbani, kununua nafaka moja kwa moja kutoka mashambani.
Data ya serikali inaonesha kwamba kati ya 2022 na 2025, takriban sampuli moja kati ya sita za chakula zilizopimwa na mamlaka zilishindwa kufikia viwango vya usalama wa chakula. Katika kipindi hicho hicho, zaidi ya leseni 1,100 za biashara za chakula zilifutwa.
Wataalamu wanasema kesi hizi zinaweza kusababishwa na chochote kuanzia usafi duni na ukiukwaji wa nembo hadi kesi zinazohusisha uchafuzi au uchakachuaji.
Mwezi uliopita, maafisa wa usalama wa chakula huko Hyderabad walikamata zaidi ya kilo 3,000 za unga wa chai uliochanganywa ambapo rangi za sintetiki, juisi ya tangawizi na chai iliyoisha muda wake zilichanganywa ili kuongeza mwonekano ili kupata faida, The Indian Express iliripoti.
Uchakachuaji wa chakula si jambo jipya nchini India. Lakini mfumo wa udhibiti unaojitahidi kuendana na uchumi mkubwa usio rasmi wa chakula, na mitandao ya kijamii inayoeneza vitisho vya usalama wa chakula haraka kuliko mamlaka zinavyoweza kujibu, vimeungana na kusababisha mgogoro unaokua wa duala la uaminifu.
Miongo michache iliyopita, uchakachuaji wa chakula ulimaanisha maziwa yaliyopunguzwa au kokoto kwenye nafaka. Leo, uvamizi huleta maziwa yaliyotiwa sabuni na viungo vilivyotiwa rangi.
India ina sheria za kuzuia hali hii. Mamlaka ya Usalama wa Chakula na Viwango nchini India, (FSSAI), iliyoundwa chini ya sheria ya mwaka 2006, inadhibiti jinsi chakula kinavyotengenezwa, kuhifadhiwa, kusafirishwa na kuuzwa, ikichukua nafasi ya mkusanyiko wa sheria za zamani zilizokuwepo hapo awali.
Kwa mujibu wa sheria hizo, kila kitu kuanzia kampuni kubwa za chakula hadi migahawa midogo lazima kipate leseni, huku maafisa wa usalama wa chakula wakipewa jukumu la kufanya ukaguzi, kukusanya sampuli na kuchunguza malalamiko.
"Ni mojawapo ya sheria za kisasa zaidi za usalama wa chakula duniani," anasema Pawan Agarwal, aliyekuwa mkuu wa FSSAI. "Inaweka viwango vya wazi kuhusu jinsi chakula kinavyopaswa na kisivyopaswa kuuzwa."
Lakini kwa vitendo, sheria hizo mara nyingi huanza kutekelezwa kikamilifu baada ya tatizo kutokea tayari.
"Kampuni kubwa zinatarajiwa kupima bidhaa kabla hazijaingia sokoni, lakini sehemu kubwa ya mfumo wa biashara ya chakula haifanyi kazi kwa namna hiyo," alisema Agarwal.
"Bidhaa za chakula mara nyingi hupimwa tu baada ya malalamiko kutokea au mashaka kuibuka."
Kufikia wakati huo, bidhaa zilizochakachuliwa zinaweza kuwa tayari zimesambazwa katika miji au majimbo mbalimbali.
Pia anaeleza changamoto inayotokana na bidhaa za chakula zinazouzwa bila vifungashio rasmi, kama mafuta, unga na viungo vinavyouzwa kwa kiasi kidogo bila chapa maalum.
Kote India, wauzaji wadogo wengi, maduka yasiyosajiliwa na viwanda visivyo rasmi huuza, hupakia upya na kusambaza bidhaa hizo bila nyaraka za kutosha, jambo linalofanya iwe vigumu kufuatilia bidhaa zisizo salama zilipotoka au zilipoishia, wataalamu wanasema.
Wakati huohuo, mfumo wa upimaji wa chakula una dosari ya kimuundo pia, anasema Saurabh Arora, mkurugenzi mkuu wa maabara ya kupima chakula ya Auriga Research.
"Biashara zinatakiwa kupeleka sampuli mara moja tu kila baada ya miezi sita au 12. Lakini hata muda huo mdogo wa upimaji hupangwa kwa ujanja," anaongeza.
"Mara nyingi wanahakikisha kundi linalopimwa linafikia viwango vinavyotakiwa, hata kama mengine hayafikii."
Wataalamu wanasema uwezo dhaifu wa utekelezaji wa sheria ni changamoto nyingine kubwa.
Katika jimbo la Maharashtra, moja ya majimbo makubwa zaidi India, maafisa wa usalama wa chakula wasiozidi 500 wanasimamia maelfu ya biashara zilizosajiliwa pamoja na waendeshaji wengi wasio rasmi, anasema mtaalamu wa usalama wa chakula Sanjay Indani, ambaye amewahi kufanya kazi na mdhibiti huyo.
"Ni vigumu kusimamia kila kitu. Inawezekanaje idadi ndogo kiasi hicho ya maafisa kuwawajibisha watu wote?"
Wataalamu wanasema nchi kama Italia na Uingereza zinaweza kufuatilia na kuondoa bidhaa sokoni haraka kupitia mifumo ya usambazaji. India, kwa upande mwingine, kufuatilia bidhaa zisizo na ubora kunaweza kuchukua wiki kadhaa.
Ukubwa wa tatizo hilo umefika hadi katika ofisi za juu serikalini. Mwezi uliopita, Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu, ilifanya mkutano kuhusu usalama wa chakula, ambapo maafisa walionya kuwa bidhaa zilizochafuliwa zinaweza kusambaa kwa kiwango kikubwa kabla mamlaka hazijazibaini au hata kuziondoa madukani.
Lakini kwa wananchi wengi wa kawaida, suluhisho limekuwa rahisi zaidi, kulipa zaidi ili kuwa na wasiwasi mdogo.
Tiash De, mwenye umri wa miaka 29 anayeishi jijini Mumbai, anasema hofu ya bidhaa zisizo na viwango imemsukuma kununua bidhaa za gharama kubwa zaidi.
"Mara nyingi nachagua bidhaa za kampuni kubwa, ingawa ni ghali na zinaongeza mzigo kwenye bajeti yangu, lakini kichwani naamini hazijachakachuliwa," anasema.
Pia hulipa karibu 50% zaidi ya bei ya kawaida ya soko kwa huduma ya kupeleka maziwa moja kwa moja kutoka shambani hadi nyumbani, gharama ambayo anasema inafaa kwa amani ya moyo anayopata.
Yeye si peke yake. Katika miji mbalimbali ya India, watumiaji wengi zaidi wako tayari kulipa gharama ya ziada kwa chakula kinachoaminika, huku soko la chakula hai (organic food market) nchini humo likitarajiwa kufikia dola bilioni 10.81 ifikapo mwaka 2033, kwa mujibu wa Dr Meenakshi Singh, mwanasayansi mkuu katika Council of Scientific and Industrial Research (CSIR).
Madaktari wanasema hatari kubwa zaidi mara nyingi hutokana na chakula ambacho hakisababishi watu kuugua mara moja. Tofauti na sumu ya chakula, ambayo husababisha ugonjwa wa ghafla, kuendelea kutumia viambato vilivyochafuliwa au visivyo na viwango kunaweza kuchukua miaka mingi kabla madhara yake kuonekana.
"Kwa muda mfupi, watu wanaweza kupata matatizo ya mmeng'enyo wa chakula, maumivu ya kichwa au uchovu," anasema Rinkesh Kumar Bansal, mkuu wa kitengo cha magonjwa ya mfumo wa chakula katika hospitali ya Fortis karibu na Delhi.
"Baada ya muda, hali hiyo inaweza kuchangia uharibifu wa ini na figo, matatizo ya homoni na kuongeza hatari ya magonjwa sugu."
Lakini wataalamu wanasema hofu ya sasa inachochewa zaidi na taarifa zinazosambazwa mtandaoni kuliko ongezeko halisi la magonjwa.
"Uchakachuaji wa chakula haujaongezeka ghafla, lakini taarifa zake sasa zinasambaa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii," anasema Pawan Agarwal.
"Tunajali sana chakula tunachokula na ni jambo la binafsi kwetu, hivyo habari kama hizi husabisha sisi kuwa makini mara moja."
Anasema shinikizo la kweli mwishowe litatoka kwa watumiaji wenyewe.
"Kadiri uelewa unavyoongezeka na watu wanavyoanza kudai chakula salama zaidi, biashara hazitakuwa namna nyingine isipokuwa kuboresha ubora."
Pia alionesha ishara moja ya mabadiliko, Food Safety and Standards Authority of India (FSSAI) mara kwa mara huchapisha mwongozo wa jinsi ya kugundua chakula kilichochakachuliwa nyumbani, jambo ambalo anasema ni nadra katika sehemu nyingine duniani.
"Lazima kuwe na hisia ya uwajibikaji kuanzia kwa mtengenezaji hadi kwa mlaji," anaongeza Saurabh Arora.
"Nchini India, mara nyingi mtazamo huwa, mradi mimi sili bidhaa hiyo, basi ni tatizo la mtu mwingine. Sheria pekee haziwezi kutatua hilo."
Huko jikoni kwa Rao mjini Delhi, sasa mitungi ya viungo vya kutengenezwa nyumbani imejaa kwenye rafu iliyokuwa ikitumiwa kuhifadhi pakiti za viungo vya dukani.
Anakubali kuwa mchakato huo unachukua muda mwingi na si rahisi kwa vitendo, hasa kwa familia ambazo wazazi wote wana kazi za muda wote.
"Kama hata chakula cha msingi hakiwezi kuaminika, watu wa kawaida wanapaswa kufanya nini?"